12 November 2010

Mancini akana kutafuta sare.

LONDON, England

KOCHA Roberto Mancini, amesema timu yake ya Manchester City ilikuwa haichezi kwa ajili ya kutafuta sare katika mchezo wao na wapinzani wao wakuu
Manchester United katika michuano ya Ligi Kuu ya England.

Katika mtanage huo wa juzi, uliofanyika kwenye Uwanja Eastlands wenyeji hao walionekana kuimarisha zaidi safu ya ulinzi tofauti na ilivyokuwa majirani zao.

Hata hivyo pamoja na ulinzi huo na ushindani mkali, mechi hiyo ilimalizika kwa matokeo ya sare.

 Katika mchezo huo maswali yalianza kuibuka baada ya Mancini, kuamua kumtumia mshambuliaji Carlos Tevez peke yake mbele lakini, Muitaliano huyo anadai hakudhamiria kuaribu mchezo akisema alifanya hivyo kutokana na uwezo aliokuwa nao mchezaji huyo katika safu ya ushambuliaji.

"Unapocheza dhidi ya Manchster  United ni rahisi kupoteza mchezo kwa sababu utakapowapa nafasi ya kufunga watakufunga," Mancini aliiambia Sky Sports.

"Nilitaka kushinda mechi hii, ila ni vizuri zaidi kutoka sare kuliko kufungwa kama ilivyokuwa mwaka jana tulitaka tushinde mechi hii," alisema kocha huyo.

Katika mechi iliyozikutanisha timu hizo msimu uliopita, mchezaji Paul Scholes alifunga bao dakika za mwisho lililoipa pointi tatu Manchester United na kocha, Mancini anaamini tangu kipigo hicho kikosi chake kimeboreka na hakuna aibu kwa kutoka suluhu kwenye uwanja wake wa nyumbani ikilinganishwa na kiwango cha Manchester United.

"Nadhani ulikuwa ni mchezo mgumu kwa timu zote mbili. Nafakiri matokeo ni sahihi," alisema.

No comments:

Post a Comment