24 November 2010

Mamia wapoteza maisha katika msongamano Cambodia.

PHNOM PENH,Cambodia.

WAZIRI Mkuu wa Cambodia,Bw.Hun Sen amesema kuwa watu wapatao  345 wamepoteza maisha katika msongamano wakati wa maadhimisho ya sikukuu muhimu  katika mji mkuu wa
nchi hiyo, Phnom Penh.

Waziri Mkuu huyo alisema jana kuwa watu hao walikufa juzi baada ya umati mkubwa kukusanyika katika kisiwa kidogo siku ya mwisho ya maadhimisho ya Tamasha la Maji ambayo ni moja matukio makubwa kufanyika kila mwaka nchini humo.

Alisema,  msongamano huo ulitokea darajani ambako mashuhuda wanasema kuwa kulikuwepo na umati mkubwa wa watu huku mamia wakiwa wamejeruhiwa.

Waziri Mkuu  Sen alilielezea tukio hilo kuwa ni kubwa kuikumba  Cambodia tangu yalipotokea mauaji yaliyofanywa na utawala wa  Bw.Khmer Rouge miaka ya 1970.

Alisema,tayari wameagiza ufanyike uchunguzi na atatangaza siku ya maombolezo baadaye wiki hii na pia ameziagiza  wizara zote za serikali zipeperushe bendera  nusu mlingoti.


Msemaji wa Serikali, Bw.Khieu Kanharith aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa watu zaidi ya  400 wamejeruhiwa katika tukio hilo.


"Vifo vingi ni matokeo ya kukosa hewa na majeraha ya ndani kwa ndani,"alisema.

Serikali inakadiria kuwa watu zaidi ya milioni mbili walihudhuria sherehe hizo za siku tatu.



Ilielezwa kuwa msongamano huo ulianza baada ya kumalizika tamasha hilo lililokuwa likifanyika katika kisiwa cha  Diamond ambazo ufuatiwa na mbio za boti katika mto  Tonle Sap kuashiria kumalizika sikukuu hiyo.


Raia wa Australia,Bw.Sean Ngu ambaye alikuwa nchini Cambodia kutembelea familia na marafiki zake  ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC kuwa watu wengi walikuwa eneo la  darajani.

Alisema, baadhi ya walioathirika walipigwa na shoti ya umeme.

"Kulikuwepo na watu wengi darajani na wote waliishia kusukumana,"alisema na kuongeza kuwa jambo hilo lilisababisha taharuki miongoni mwaoa jambo ambalo lilisababisha watu waliokuwa katikati kuanguka chini na kisha kuanza kukanyagana.

Iliripotiwa kuwa hospitali ya Calmette ambayo ndiyo hospitali kuu ya mji wa  Phnom Penh imejaa maiti na majeruhi hali ambayo imelazimisha baadhi ya majeruhi kutibiwa maeneo ya wazi.

No comments:

Post a Comment