22 November 2010

Kili Stars kuikabili Kenya leo.

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', leo itajitupa uwanjani kumenyana na Kenya 'Harambee Stars' katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam.

Awali mchezo huo ulitakiwa kupigwa Jumatato iliyopita, ambayo ilikuwa ni siku ya maalumu katika kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), ipigwe michezo ya kimataifa duniani.

Lakini kukosekana mapema kwa timu ya kujipima na Kilimanjaro Stars, ndiyo iliyosababisha mchezo huo upigwe leo ikiwa pia ni sehemu ya mandalizi ya mashindano ya Kombe la Chalenji.

Harambee Stars inakuja nchini kwa mara ya pili mwaka huu, kwani awali ilicheza na timu ya taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 'Taifa Stars' katika huo na kutoka sare ya bao 1-1.

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro, Jan Poulsen ambaye pia ni kocha wa Taifa Stars, alisema kikosi chake kipo vizuri kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

"Ni mchezo wa kujipima nguvu, lakini kwetu sisi utakuwa na maana nyingi ikiwa ni pamoja na kutafuta wachezaji watakaoiwakilisha nchi katika mashindano ya Chalenji na pia kuwadhihirishia Wakenya, kwamba sasa tumebadilika," alisema Poulsen.

Alisema kuwasili kwa Henry Joseph, anayecheza soka la kulipwa nchini Norway katika Klabu ya Kongsvinger na Idrissa Rajabu wa SOFAPAKA ya Kenya, kutaisaidia timu hiyo kufanya vizuri katika michezo yake.

1 comment:

  1. kila la heri kili stars.wachezaji wanapaswa kujua watanzania wanahitaji matokeo mazuri. timu ikifanya vizuri kwenye mechi hii itaongeza hari ya mashabiki

    ReplyDelete