22 November 2010

Gulam akiri riadha kuwa na mfumo mbovu.

Na Amina Athumani.

RAIS wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Rashid Gulam amekiri mfumo mbovu wa riadha uliopo kwa sasa na kwamba Tanzania, inaweza kuchukua miaka 10 na zaidi kutwaa medali
katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Gulam alisema historia ya riadha kwa sasa nchini imetoweka kabisa kutokana na mfumo mbovu wa mchezo huo na kwamba mikakati na mipango thabiti inahitajika, ili kurudisha hadhi na heshima iliyopotea katika mchezo huo.

"Riadha ndiyo mchezo wa kwanza ulioiletea heshima nchi miaka ya nyuma, lakini kwa sasa historia ya mchezo huu imeharibika kabisa kutokana na mfumo wa kuibua vipaji kuwa si wa kuridhisha," alisema Gulam.

Alisema kutokana na hali hiyo, upo uwezekano wa kipindi cha miaka 10 au hata na zaidi kuweza kuwaandaa vijana wenye umri mdogo kwa kipindi cha miaka hiyo, ndiyo uwezekano wa kurudisha hadhi ya mchezo wa riadha utakapopatikana.

Alisema Kamati ya Olimpiki kupitia Kamati ya Kimataifa ya (IOC), iandae semina nyingi nchini zitakazoweza kuandaa walimu wenye viwango vya kimataifa, ili waweze kuandaa vijana wadogo kwa kipindi kirefu zaidi na kwamba nchi nyingi zinafanya vizuri katika michezo, nazo zinatumia mfumo wa kuandaa vijana wengi zaidi wenye umri mdogo kwa muda mrefu.

Alisema Serikali pia nayo inatakiwa kusaidia katika suala hilo, kwani semina nyingi zinazoendeshwa zinakuwa hazina vifaa vya mchezo husika, hivyo kufanya walimu kufundishwa bila ya vitendo.

No comments:

Post a Comment