22 November 2010

Diwani aomba ushirikiano Kinyelezi.

Na Mohamed Kazingumbe

DIWANI Mteule wa CCM, Kata ya Kinyelezi katika Halmashauri ya Ilala, Bi. Leah Mgitu ameomba ushirikiano wa karibu wa wapiga kura wake ili kufanikisha ahadi zake kwa wananchi.
Aliyasema hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hizo kuhusu mipango na mikakati yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.

"Najua kata yangu ni miongoni mwa kata zinazokua kwa kasi sana katika Halmashauri ya Ilala pia katika jiji letu la Dar es Salaam,lakini changamoto kubwa ni namna gani wapiga kura wangu watakuwa wawazi na wepesi katika kuchangia hoja za maendeleo ya kata yetu," alisikika akieleza mara baada ya matokeo.

Huku akiwashukuru wananchi kwa kumpa ridhaa ya kuwa kiongozi wao, alitaja kipaumbele katika suala zima la elimu kuwa atashirikiana na wazazi kuona suala la walimu na wanafunzi linatatuliwa linapojitokeza kupitia kamati za shule.

"Naelewa wananchi wangu wangependa maendeleo ya haraka, lakini nitapenda kuchukua changamoto zao na mikakati ya muda mrefu tuzifanyie kazi pamoja tuone mambo gani yatatakiwa nguvu za serikali kuu na zipi zinazohitaji nguvu za wananchi wenyewe," alisema.

Akizungumzia uchaguzi uliompa ushindi, alisema, "Kazi ilikuwa ngumu sana na iliyostahili ujasiri mkubwa kukabiliana na misukosuko ya wapinzani".

Katika suala la mikopo na uanzishaji wa vikundi vya kimaendeleo wa wajasiriamali wadogo, alitamka juu ya kuhamasisha kujiunga katika SACCOS na uanzishaji wa vikundi vya uzalishaji.

Wakichangia hoja juu ya nini wanategemea kutoka kwa diwani wao, wakazi wa Kinyelezi walitaka kipaumbele kwake kiwe uadilifu juu ya rasilimali ya kata yao.

Kauli hiyo inakuja baada ya kubainika kuwa uwakilishi uliopita katika nafasi hiyo ulikumbwa na tuhuma za kashifa za matumizi mabaya ya ofisi.

No comments:

Post a Comment