LONDON, England.
KOCHA wa Chelsea, Carlo Ancelotti amewapongeza wachezaji wake, licha ya timu hiyo kupata kipigo cha bao 1-0 bila kutarajia kutoka kwa timu ya Birmingham City.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu, walifungwa kutokana na jitihada za mchezaji Lee Bowyer, katika kipindi cha kwanza lakini shujaa halisi katika mchezo huo alikuwa ni kipa, Ben Foster ambaye pia anadakia timu ya taifa ya England, kuokoa mabao mengi na kuinyima Chelsea ushindi.
Ushujaa huo wa Foster, ndiyo uliiokoa timu hiyo ya Magharibi mwa London, isiambulie kipigo cha tatu kati ya mechi nne za ligi na kuifanya Chelsea kuendelea kubaki kileleni mwa ligi kwa tofauti ya magoli.
Chelsea tayari ilishalazwa mabao 3-0 na Sunderland ikiwa nyumbani kwenye uwanja wake wa Stamford Bridge, mechi iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita lakini, Ancelotti alisema kwa sasa anaona timu yake imeongezeka kiwango.
Aliiambia Sky Sports: "Tunaweza kujibu vizuri mashambulizi. Tumecheza mpira mzuri kwa dakika zote 90 na tuna moyo mzuri wa kujituma na hali nzuri.
"Tumefadhaishwa na matokeo, lakini nadhani jambo hilo ni kawaida kwasababu nadhani tulistahili kushinda," aliongeza kocha huyo na kuongeza kuwa walistahili kufungwa na Sunderland, lakini kwa juzi walistahili kuondoka na ushindi ingawa anadhani walikosa bahati ila akasema kuwa hilo ndilo soka.
Mbali na kujiliwaza huko, kocha huyo alimwagia sifa mlinda mlango Foster kwa kiwango alichoonesha na kuokoa mabao mengi, akisema kuwa anampongeza sana.
"Didier Drogba alicheza mechi vizuri na alipata nafasi nyingi, lakini hakuwa na bahati ndiyo maana akawa anagonga miamba," alisema.
No comments:
Post a Comment