19 November 2010

AMI yazindua kampeni upimaji kisukari.

Na Elisante Kitulo

KATIKA kuadhimisha mwezi wa kuhamasisha ulimwengu kuhusu ugonjwa wa kisukari, Hospitali ya AMI imeanzisha kampeni ya kushawishi wananchi kujenga utaratibu wa
kupima damu ili kujua kiwango cha sukari, ikiwa ni hatua muhimu ya kukabiliana na ugonjwa huo nchini.

Kampeni hiyo pia itahusisha huduma ya kupima kisukari na shinikizo la damu bure kuanzia Jumatatu, Novemba 22, huduma ambayo itatolewa hospitalini hapo hadi mwisho wa mwezi huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Amit Thakker alisema wameamua kuanzisha kampeni hiyo baada ya ugonjwa huo kuzidi kuenea barani Afrika huku wengi wakiwa hawana uelewa wa kutosha juu yake.

"Ukizingatia mwezi Novemba ni mwezi wa kuhamasisha ulimwengu kuhusu ugonjwa wa kisukari, hospitali yetu imeanzisha kampeni itakayohamasisha jamii kupima na kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa huo.

"Idadi ya watu wanaotambulika kuugua kisukari katika nchi maskini ni nusu ya idadi ya watu wanaokadiriwa kuwa na ugonjwa huo," alisema.

Alisema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa watu milioni 285, ambayo ni sawa na asilimia 6.4 ya watu duniani wanaishi na ugonjwa wa kisukari.

Dkt. Thakker alisema nchini Tanzania watu 500,000 wanakadiriwa kuishi na kisukari, huku vifo 15,408 vinatokana na ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment