28 October 2010

Toto African yatamba kuizabua Yanga.

Na Addolph Bruno

TIMU Toto African ya Mwanza, imetamba kuifunga Yanga katika mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza, ikiwa watacheza katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Novemba 7 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Nofli Omary alisema kutokana na kuwa na wachezaji waliozoea hali ya hewa tofauti msimu huu, watafanya vizuri katika mchezo huo.

"Nafikiri baada ya taratibu za uchaguzi kukamilika uwanja wa Uhuru utakuwa tayari kutumika, timu yetu itawasili Dar es Salaam mara moja kuikabili Yanga kwa mbinu zote na hakika tutashinda," alisema Omary.

Alisema walishindwa kufanya vizuri msimu uliopita katika baadhi ya mechi zao kutokana na kusajili wachezaji mchanganyiko, walioshindwa kuonesha uwezo uwanjani.

Mwenyekiti huyo alisema asilimia kubwa ya wachezaji wanaoichezea klabu hiyo msimu huu, wametoka katika maeneo ya kanda ya Ziwa ambao alidai wanaweza kumudu hali ya hewa sehemu yoyote.

Alisema ikiwa Uwanja wa Uhuru utaanza kutumika mapema kabla ya Novemba 7, Toto itawasili Dar es Salaam Novemba 5, mwaka huu kujiandaa na mchezo huo.

No comments:

Post a Comment