27 October 2010

Darasa la saba kuingia sekondari bila mchujo.

*Serikali kuajiri walimu wapya 19,204 Novemba.
*Prof. Magembe atamba elimu bure ni sera ya CCM.

 
Na Mwandishi Wetu, Mwanga

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe amesema serikali inafanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na
wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba kuendelea na kidato cha kwanza hadi cha nne bila kuchujwa.

Prof. Maghembe alitoa kauli hiyo jana kwenye mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake mjini Mwanga mkoani Kilimanjaro na kufafanua kuwa mabadiliko hayo yanamaanisha kwamba ukomo wa elimu ya msingi kwa Tanzania sasa utakuwa kidato cha nne kuanzia mwaka 2012.

"Msingi wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010 ni kuwa kuanzia mwaka 2012, elimu ya msingi itakuwa ni kuanzia chekechea hadi kidato cha nne," alisema na kuongeza;

"Kinachofanyika sasa ni marekebisho katika shule za sekondari ili kuziwezesha kila shule ya kata kuwa na chumba chenye kusubiri watakaohitimu darasa la saba kwa ajili ya kuingia kidato cha kwanza. Hivyo Watanzania wote watasoma hadi kidato cha nne, na hii ndiyo itakayo kuwa elimu yetu ya msingi," alisema Profesa Maghembe. Kwa sasa elimu ya msingi ya Tanzania inaishia darasa la saba.

Kauli hiyo ya Profesa Maghembe inakuja wakati kukiwa na joto la kampeni, ambapo sera za baadhi ya vyama vya upinzani zimeweka wazi kuwa wakichaguliwa elimu ya msingi itakuwa hadi kidato cha sita na itagharamiwa na serikali.

Prof. Maghembe alisema shule zote za sekondari za kata, zinaagizwa kujenga madarasa yake kulingana na idadi ya wanafunzi waliomo katika shule za msingi ndani ya kata husika.

Kuhusu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ambao hutumika kuwachuja wanafunzi wanaondelea na masomo ya juu na wale ambao hawakufaulu, alisema mtihani huo utaendelea kuwapo lakini hautakuwa wa mchujo bali ni wa kupima maarifa tu kama ule wa kidato cha pili.

"Mtihani huo hautakuwa wa kuwabagua wanafunzi wa kuendelea na sekondari na wengine wa kubaki. Badala yake utapima maarifa waliyoyapata wanafunzi katika kipindi cha miaka saba. Watoto wote watakaomaliza darasa la saba, wataendelea na kidato cha kwanza hadi kumaliza kidato cha nne kulingana na uwezo wa kila mwanafunzi," alisema Prof. Maghembe.

Alisema shule za sekondari zitaongezewa uwezo tangu mwaka huu kwa kila moja kupatiwa walimu watano ambao watahitimu katika vyuo vya elimu vinavyotoa stashahada na shahada. Novemba hii serikali itaajiri walimu wapya wapatao 19,204 wakiwamo wa shahada na stashahada.

Alisema katika mpango huo wa kuimarisha shule za sekondari, kila shule itajengewa maabara ya sayansi na kupatiwa vifaa vya maabara hizo.

Akizungumza katika mahojiano hayo, Prof. Maghembe ambaye pia ni mgombea ubunge katika Jimbo la Mwanga alisema ndani ya miaka mitatu, matatizo ya walimu, maabara, vitabu na nyumba za walimu katika sekta ya elimu yatakuwa historia.

Prof. Maghembe alisema serikali imeuisha sera tatu zilizokuwa zinaendesha na wizara inayosimamia elimu, ambazo ni; Sera ya Elimu na Mafunzo, Sera ya Ufundi na Ufundi Stadi na Sera ya Elimu ya Juu.

Badala yake imeundwa sera moja inayofahamika kama Sera ya Elimu na Mafunzo, ambayo itaanza kutumika mwaka 2011/2012. Sera mpya itaweka dira ya elimu itakayolenga ubora wa elimu katika ngazi zote ambazo ni msingi, sekondari, ualimu, elimu ya juu na elimu ya ufundi na ufundi stadi.

Sera hii mpya inalenga asilimia 30 ya wanafunzi wanaotarajiwa kuingia sekondari wapatao milioni nne kwenda kidato cha tano na cha sita ifikapo 2015 na asilimia 12 ya vijana hao kwenda chuo kikuu, kiwango ambacho kinakubalika kimataifa katika misingi ya maendeleo.

Hata hivyo, wakati juhudi hizo zikiendelea kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, idadi ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne imeongezeka kutoka 128,917 mwaka 2005 na kufikia 485,054 mwaka 2010.

Kwa kidato cha nne hadi mwaka 2004 walikuwa wanahitimu wanafunzi 22,304, lakini kwa mwaka huu wamehitimu wanafunzi 65,629 (kati ya hawa watahiniwa wa shule ni 42,000 na waliosalia ni watahiniwa binafsi) na idadi inazidi kuongezeka.

Kwa upande wa vyuo vikuu wakati jumla ya wanafunzi wote walioandikishwa walikuwa ni 37,000 katika ngazi ya shahada mwaka 2004, mwaka 2010 ngazi hiyo ya shahada walioandikishwa ni 117,000. Ukijumlisha wanafunzi hawa na wanafunzi walioandikishwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu hapa nchini kwa masomo ya diploma na diploma za juu, jumla ya wanafunzi waliodahiliwa mwaka 2010 katika ngazi ya elimu ya juu inakaribia 350,000.

Kuhusu tatizo la upungufu wa walimu, Prof. Maghembe alisema tatizo hili baada ya miaka mitatu litakuwa historia. Kwa mwaka huu idadi ya walimu waliohitimu kwa ngazi ya cheti ni takribani walimu 14,000 na tayari wamepangiwa kufundisha katika mikoa mbalimbali.

Kwa kwa ngazi ya diploma walimu 7,084 wamehitimu mwaka huu na kwa ngazi ya shahada walimu 12,120 wamehitimu mwaka huu. Ongezeo hili la walimu linatokana na kupanua mafunzo ya ualimu katika vyuo vya ualimu na kuongeza vyuo vikuu vinavyotoa mafunzo ya ualimu.

Akielezea tulikotoka, Waziri Maghembe, alisema mwaka 2005 walimu waliohitimu ngazi ya shahada walikuwa 603, wakati waliohitimu mwaka huu ni 12,120. Hawa wote wanaajiriwa na Serikali Novemba mwaka huu na wataziba pengo kubwa la walimu lililopo.

Kwa sasa kuna upungufu wa walimu 38,000 kwa shule za msingi na walimu 54,000 kwa shule za sekondari, lakini kutokana na mpango alioueleza Prof. Maghembe wa kila mwaka kuhitimu walimu 14,000 wa shule za msingi na walimu 19,200 wa shule za sekondari, ni wazi kufikia mwaka 2013, tatizo hili litakuwa historia.

Serikali imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha inapata walimu wa kutosha ambapo mbali na kuvipandisha hadhi vyuo vya ualimu vya Chang’ombe Dar es Salaam na Mkwawa Iringa, imejenga Chuo Kikuu cha Dodoma, kinachozalisha walimua 10,000 kwa wakati mmoja, sasa vipo vyuo vikuu 17 nchini vyenye kutoa shahada za ualimu.

Wakati mwaka 2005 Tanzania ilikuwa na jumla ya sekondari 1,745, Serikali ya Awamu ya Nne imejenga sekondari kila kata na kufikisha idadi ya sekondari 4,266 kwa nchi nzima. Kati ya hizo sekondari 3,300 ni za Serikali na zinazosalia ndizo za watu binafsi na mashirika ya dini.

Wakati huo huo Prof. Maghembe alisema kuwa Sera ya Kutoa Elimu bure ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kimekuwa kikiitekeleza kwa vitendo tangu mwaka 2002. 

Alisema mwaka 2002, Serikali ilifanya uamuzi wa kufuta ada kwa shule za msingi, ikapunguza ada kwa elimu ya sekondari kutoka sh. 40,000 hadi Sh. 20,000 na baadaye ikafuta ada za mitihani ambazo zilikuwa zikiwafanya watoto wengi kushindwa kuhitimu masomo ya kidato cha nne.

Mwaka 2008 wanafunzi 40,000 walishindwa kufanya mitihani ya kidato cha nne kwa kushindwa kulipa ada za mitihani, kitu kilichoifanya Serikali kufuta ada hizo.

“Elimu ya msingi haina ubishi ni bure kwa miaka yote minane, kuanzia chekechea hadi darasa la saba. Huyu anayesoma sekondari, tumepunguza hadi Sh. 20,000, tena tukasema alipe mara mbili kwa mwaka kwa maana ya Sh 10,000 kila baada ya miezi sita. Hii ina maana mtu akifuga na kuuza jogoo wawili kwa mwaka, tayari anasomesha mtoto wake,” alisema.  

No comments:

Post a Comment