Na Tumaini Makene
MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa amelipua bomu jingine, akitumia nyaraka anazodai walizikamata hivi karibuni zikidai kuwa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejiandaa kutumia vijana wake wanaoitwa 'Green Guards', kufanya vurugu na kuhatarisha amani nchini kwa kupiga wananchi.
Dkt. Slaa katika madai hayo mapya amesema kuwa kama vijana hao wataendekezwa kufanya vitendo hivyo bila kukemewa wala kudhibitiwa na mamlaka za juu serikalini na ndani ya CCM, wataiweka amani ya nchi katika hatihati, hususan wakati huu wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Mgombea huyo alisema hayo jana Viwanja vya Mwembe Yanga, Dar es Salaam wakati akihutubia umati mkubwa katika mfululizo wa mikutano yake ya kampeni...
"Nimeshasema katika mikutano yangu karibu yote niliyohutubia mpaka sasa ambako kila mahali nimekuwa nikizungumzia suala la amani...amani haihubiriwi tu majukwaani, amani inatengenezwa...mazingira ya amani yanatengenezwa."
"Sasa ngoja niwasomee nyaraka hapa, ili mjue kuwa CHADEMA ni chama makini tunaweza kujilinda...karibuni tukiwa Mwanza tulikamata nyaraka katika gari moja lililoingilia msafara na kuleta vurugu, tulikuta nyaraka zinazoonesha kuwa CCM wamejiandaa kufanya fujo kupitia vijana wa Green Guard," alisema Dkt. Slaa na kuongeza.
"Tulikuta nyaraka zikisema wameajiri vijana 50 wa Green Guards, kila mmoja atalipwa sh. 5,000, kila mmoja atanunuliwa vifaa vya kazi kama spray, pia watanunua pingu mbili...kwa wale wasiojua spray ni dawa fulani ya maji unayopuliziwa usoni, machoni na yanawasha kama pilipili."
Kwa mujibu wa Dkt. Slaa, dawa hiyo iliwahi kutumiwa kuwaumiza wafuasi wa CHADEMA katika chaguzi ndogo za Kiteto na Biharamulo, huku pia akihoji uhalali wa vijana wa chama cha siasa kupanga kununua pingu wakati ni kifaa kinachotakiwa kutumiwa au kumilikiwa na Jeshi la Polisi.
Alirudia kauli yake ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete, ambaye mbali ya kuwa mgombea urais wa CCM, pia ni mwenyekiti wa chama hicho, aoneshe kwa dhati kupinga kuhatarishwa amani ya nchi kwa kukemea vitendo vya 'Green Guards'.
"Dawa hiyo ya 'spray' ilitumika dhidi ya vijana wangu wakiwa kituo chga polisi huko Kijungu Kiteto, wakiwa kituoni...pia ilitumika huko Biharamulo, katika uchaguzi mdogo, nyote mnajua pingu ni chombo cha polisi kukamatia wahalifu...narudia kutoa kauli ya kumtaka Rais Kikwete...
"Yeye bado ndiye mwenye dhamana ya amani ya nchi hii, hakuna chama kingine tofauti na CCM kinaweza kuvuruga amani ya nchi hii, amani ya nchi hii ikivurugwa Kikwete atabeba dhamana, akiwa rais na mwenyekiti wa chama akemee vitendo hivi.
"Vijana hawa wameandaliwa katika makambi, wanapewa mafunzo ya ukakamvu ambayo ni ya kijeshi, wananaadaliwa kwenda kuwapiga vijana wenzao, tayari wameshafanya hivyo maeneo mbalimbali, wanapiga raia wasiokuwa na hatia...sasa kila chama kikiwa na jeshi la namna hii, nchi haitakalika," alisema Dkt. Slaa.
Akizungumzia sera za chama chake katika kuinua maisha ya watu wa wa kawaida, Dkt. Slaa aliahidi kufanya maboresho jeshini kwa kuunda jeshi dogo lenye dhana za kisasa na maslahi bora kwa wapiganaji wa ngazi zote, tofauti na sasa ambapo maafisa juu ndiyo wanaonekana kufaidi.
Pia alisema kuwa katika moja ya mabadiliko ya katiba hususan kipengele cha kupunguza madaraka ya rais, atahakikisha wateule wa rais wanajadiliwa na kuthibitishwa na bunge, kwa niaba ya wananchi.
Dkt. Slaa ambaye alisema kuwa huo ulikuwa mkutano wake wa kuwaaga wananchi wa Dar es Salaam kabla ya kuhitimisha kampeni zake mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki, alieleza kuwa sera za chama chake zinalenga katika kusimamia maendeleo ya watu, hivyo atakuwa tayari kuhakiksha matumizi ya viongozi wakubwa serikalini yanapunguzwa ili fedha zitakazookolewa zitumike katika shughuli za maendeleo.
Alisisitiza juu ya uwezekano wa kuondoa umasikini kwa kutoa elimu ya bure, kuondoa kodi za serikali katika vifaa vya ujenzi kama vile saruji na bati ili wananchi waondokane na makazi yasiyofaa kwa kujenga nyumba bora.
Mapema akizungumza kabla ya Dkt. Slaa, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na wakili maarufu nchini Bw. Mabere Marando alisema kuwa hoja kuu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni ufisadi, hivyo watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kuchagua kiongozi anayepinga uovu huo kwa dhati, kwa vitendo.
No comments:
Post a Comment