27 October 2010

CCM ndio walikodi gari si Dewji-Mmiliki.

Na Mwandishi Wetu, Singida

HATIMAYE sakata la mgombea ubunge wa Jimbo la Singida mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Josephat Isango kudai kuwa mgombea mwenzake wa
CCM, Bw. Mohammed Dewji alikodi gari alilokuwa akitumia kwenye kampeni, limefafanuliwa baada ya mmiliki wa gari hilo kueleza kuwa alimnyang'anya kutokana na usumbufu wa malipo na kwenda kinyume na makubaliano yao.

Akizungumza na Majira nyumbani kwake jana, mmiliki wa gari hilo Bw. Saidi Madeila alisema kuwa gari hilo lilikodiwa na ofisi ya CCM Mkoa wa Singida na wala si Bw. Dewji.

"Mimi niwe muwazi kwa kweli, Dewji sijawahi kuzungumza naye kuhusu suala la gari langu na wala mtu yoyote kutoka katika ofisi yake, mimi gari nimelikodisha kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Singida baada ya kuona hawa jamaa wa CHADEMA ni wababaishaji katika suala la malipo.

"Awali tulikubaliana kuwa kila siku gari hilo litalipiwa sh. 20,000 ikiwa ni pamoja na kujaziwa mafuta na kumlipa dereva lakini nilikaa karibu wiki nzima sijalipwa fedha zangu na mbaya zaidi gari lilikua linakwenda hadi Ikungi sehemu ambayo haikuwa katika makubaliano nami," alisisitiza Madeila na kuongeza.

"Malipo yalivyokuja na kushauriana na familia yangu tukaona tusiwape tena hili gari hawa jamaa wa CHADEMA maana linakwenda kinyume na makubaliano, hata hivyo hatudaiani nao kitu chochote ndipo alifika Katibu wa CCM Mkoa Bi. Naomi Kapambala na kulihitaji gari hilo kwa ajili ya shughuli zao za chama.

Alisema baada ya kuafikiana na Katibu juu ya utaratibu mzima wa kazi, aliamua kuwapa gari hilo aina ya Suzuki Vitara lenye namba za usajili T 663 ASZ na alilipwa fedha zake zote hadi uchaguzi utakapomalizika Oktoba 31 mwaka .

Aidha Madeila alisema hivi sasa gari hilo liko chini ya ofisi ya CCM mkoa na wala halipo kwenye kampeni za Bw. Dewji kama inavyodaiwa.

“Mimi sijawahi kuzungumza na mwandishi wa habari juu ya hili gari zaidi yako leo wewe unayenihoji, nashangaa sana kusikia kuwa mimi nimezunguza na vyombo vya habari hii sio kweli uandishi wa namna hii ni wa kunichonganisha mimi pamoja na familia yangu kwa ujumla," alisisitiza.

Kwa upande wake, Bw. Dewji alieleza kusikitishwa na taarifa hizo na kwamba hajawahi kukodi gari la mtu yeyote kwa ajili ya shughuli zake za kampeni.

“Mimi nina magari yangu matatu ambayo nayatumia katika kampeni, sasa nikodi gari jingine la nini? Siwajawahi kufanya hivyo na wala sina haja ya magari mengine haya niliyonayo yananitosha na kuniwezesha kufika kila eneo na kuzungumza na wapiga kura wangu," alisema Dewji.

Hata hivyo Bw. Dewji aliwataka wananchi pamoja na wanachama wa CCM kuwa watulivu kipindi hiki na kuepuka siasa za kuchafuana badala yake wasubiri kupiga kura kwa misingi ya kistaarabu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida Bi. Kapambala alithibitisha kuwa gari hilo walikodi wao kwa ajili ya shughuli za chama na wala si Bw. Dewji kama ilivyo daiwa na kwamba mgombea huyo hahusiki kwa lolote.

“Sisi ndio tulikodi hili gari, Dewji hahusiki kabisa, yeye ana magari yake anayotumia katika kampeni zake, sasa hili la nini tena kwake?" alihoji Bi. Kapambala.

No comments:

Post a Comment