27 October 2010

Aliyefanya fujo mkutano wa CCM afa akipelekwa hospitali

Na Yvonne Mussa

MTUHUMIWA mmoja anayefahamika kwa jina la Alfred Mushi (35), fundi ujenzi mkazi wa Tegeta amefariki dunia alipokuwa akipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kuonekana ana hali
isiyoridhisha akiwa mikononi mwa polisi.

Uchunguzi wa awali kuhusu tukio hilo umebaini kwamba mtuhumiwa Alfred Mushi alikamatwa Oktoba 21, mwaka huu katika Kituo cha basi Tegeta baada ya kudaiwa alikuwa anafanya vurugu kwenye mkutano wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi CCM katika Jimbo la Kawe.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Bw. suleiman Kova alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na wenzake ambao walifanikiwa kukimbia na inadaiwa walikuwa wanatoa lugha ya matusi na kurusha mawe wakati wakiwa kwenye mkutano huo.

Alisema baada ya kukamatwa na kumfikisha katika kituo kidogo cha Polisi Tegeta na kufunguliwa jalada lenye kumbukumbu namba TGT/RB/3357/2010 na WH/IR/7844/2010 kwa kosa la kufanya fujo.

Kamanda Kova alisema mahabusu huyo wakati akiwa katika chini ya ulinzi katika kituo hicho ilidaiwa kuwa 'licha ya kuonekana kama mlevi alikuwa akifanya urugu ya kuwapiga mahabusu wenzake na hata kujibamiza kichwa na mwili wake kwenye ukuta wa mahabusu hiyo'.

Alisema kutokana na vurugu alizokuwa akifanya ambazo zilikuwa chukizo kwa mahabusu wengine askari walichukua hatua ya kumfunga pingu ili asiwadhuru wenzake, hata hivyo alikuwa anaendelea, ndipo askari kwa kushirikiana na mahabusu walimfunga kamba.

Kamanda kova alisema mnamo Oktoba 25 majira ya saa 08:00 mtuhumiwa huyo pamoja na watuhumiwa wenzake walifikishwa katika kituo cha polisi Wazo Hill kwa ajili ya kuchuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakama ya Mwanzo Kawe.

Baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Wazo, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya baada ya kumuona mtuhumiwa huyo na kupata maelezo ya kina kutoka kwa watuhumiwa wenzake, aliamuru apelekwe hospitali kwanza badala ya mahakamani.

Hata hivyo,ilipofika majira ya saa 9:00 mchana siku hiyo baada ya mtuhumiwa kufikishwa Hospitali ya Mwananyamala daktari alimchunguza na kugundua amefariki dunia.

Alisema baada ya taarifa hiyo kutolewa kwa uongozi wa Polisi Wilaya ya Kawe, jarada la kifo cha mashaka lilifunguliwa na uchunguzi kuanza kufanyika ili kubaini chanzo cha kifo hicho.

No comments:

Post a Comment