07 October 2013

YANGA YAIKAMUA MTIBWA SUGARNa Speciroza Joseph
  Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga jana wameibamiza Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Mtibwa ilianza kwa kasi ambapo dakika ya nne mshambuliaji wake Vicent Barnabas aliachia shuti kali lililookolewa na kipa wa Yanga, Ally Mustafa 'Bathez'.

Yanga ilianza kupata bao dakika ya sita kupitia kwa Mrisho Ngassa, baada ya kuwatoka mabeki wa Mtibwa na kuachia shuti lililompita kipa, Hussein Shariff.Dakika ya kumi Yanga ilifanya shambulizi langoni mwa Mtibwa ambapo, Simon Msuva aliachia shuti kali lililotoka nje ya lango.
   Mussa Hassan 'Mgosi' wa Mtibwa Sugar dakika ya 15 alikosa bao la wazi akiwa katika nafasi nzuri, lakini akajibabatiza na mpira kuwahiwa na mabeki wa Yanga.Didier Kavumbagu wa Yanga dakika ya 18 aliachia shuti kali langoni mwa Mtibwa ambapo mpira uligonga mwamba na kuokolewa na kipa wa Mtibwa.
Yanga ilipata bao la pili dakika ya 23 kupitia kwa Kavumbagu baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Msuva.Dakika ya 44 Mgosi aliikosesha Mtibwa bao, baada ya kubaki na kipa wa Yanga, lakini shuti lake likadakwa na kipa huyo, huku Kavumbagu naye akikosa bao katika dakika hiyo kutokana na shuti lake kutoka nje kidogo ya lango la Mtibwa.
  Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuingia kwa nguvu ambapo Hamis Kiiza, aliikosesha timu bao la wazi baada ya kushindwa kumalizia krosi nzuri iliyochongwa na Nizar Khalfan.Mtibwa ilizinduka dakika ya 70, baada ya Shaban Kisiga kuachia shuti kali langoni mwa Yanga ambapo mabeki waliokoa hatari hiyo.Dakika ya 72 Mtibwa ilifanya shambulizi la kushtukiza lakini shuti la mbali la Juma Luzio, liliokolewa na kipa Bathez.
  Kisiga alijaribu tena kuachia shuti kali lililookolewa na kipa wa Yanga na mpira kutoka nje ya lango. Masoud Mohamed 'Chile' aliikosesha Mtibwa bao dakika ya 84 akiwa yeye na lango lakini shuti lake likapaa nje ya lango.

No comments:

Post a Comment