16 October 2013

UPINZANI WATINGA IKULU


 
Rais Jakaya Kikwete(kulia), akisalimiana na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA),Bw. Tundu Lissu baada ya kuwasili Ikulu, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mbunge wa Kuteuliwa kwa tiketi ya Chama cha NCCR- Mageuzi, Bw.James Mbatia. Viongozi wa vyama hivyo na CUF, walikwenda Ikulu kufanya mazungumzo na Rais Kikwete juu ya mchakato wa Katiba Mpya.  
  •  WAMUANGUKIA RAIS KIKWETE ASISAINI MUSWADA WA KATIBA

 Na Eckland Mwaffisi
   Rais Jakaya Kikwete, jana alikutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni ili kujadili maendeleo ya mchakato wa Katiba Mpya nchini.

Viongozi hao waliokutana Ikulu, Dar es Salaam ambao ni Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ndiye msemaji wa viongozi hao, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bw. Philip Mangula, Bw. Isaack Cheyo aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha UDP, Bw. John Cheyo na na Mrindoko ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Bw. Augustine Mrema.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Bw. Cheyo na Bw. Mrema wako nje ya nchi. Kurugenzi hiyo iliongeza kuwa, viongozi wengine waliokuwepo katika mazungumzo na Rais Kikwete ni Bw. Habib Mnyaa, Bw. Julius Mtatiro wote kutoka CUF, Bw. Tundu Lissu, Bw. John Mnyika kutoka CHADEMA na Bw. Martin Mng'ongo wa NCCR-Mageuzi.
  Rais Kikwete alikutana na viongozi hao ili kuondoa sintofahamu iliyopo kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013, uliopitishwa na Bunge, Mjini Dodoma, hivi karibuni.
Maazimio ya kikao
  Vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kushirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria.
  Pili vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano, maridhiano ili kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi na mustakabali wa taifa.
  Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
  Katika waraka wao kwa Rais Kikwete, vyama hivyo vilimshauri atumie mamlaka aliyonayo chini ya ibara ya 97(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kutoukubali Muswada huo kwani sheria hiyo inasubiri ridhaa yake kabla ya kuanza kutumika.
  Waraka huo uliongeza kuwa, ushauri huo unatokana na imani yao kwamba, kama muswada huo utapata ridhaa yake na kuanza kutumika kama Sheria, utakuwa na madhara makubwa kwa mchakato mzima wa utungaji Katiba Mpya, kwa amani na utulivu wa nchi.
  Katika waraka huo, vyama hivyo vilisema Muswada umefanya marekebisho makubwa katika namna ya kupitisha vifungu vya Katiba Mpya katika Bunge Maalum la Katiba.
  Wakati kifungu cha 26(2) cha Sheria kama ilivyo sasa kinalazimu ili Katiba Mpya ipitishwe, sharti ikubaliwe na theluthi mbili ya wajumbe wote wa kutoka Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wajumbe kutoka Zanzibar na marekebisho yaliyofanywa kwenye Muswada huu yameondoa sharti hilo.
  Kama theluthi mbili haitapatikana ndani ya Bunge Maalum la Katiba baada ya kupiga kura mara mbili, Katiba Mpya itapitishwa kwa wingi wa kawaida wa wajumbe wote wa Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wajumbe kutoka Zanzibar.
 "Muswada huu ni mojawapo ya Muswada wa aina ya pili, yaani, Muswada ambao haukufanyiwa tafakuri ya kutosha na kuzingatia masilahi mapana ya kupata Katiba Mpya ya nchi yetu kwa njia ya mwafaka wa kitaifa na maridhiano ya wadau wote.
 "Muswada huu hautajenga maelewano kuhusu namna ya kutatua matatizo ya Muungano wetu, wala hautaziba nyufa zilizojengwa katika mchakato huu.
"Badala ya kutuunganisha, Muswada huu utatugawa zaidi badala ya kutibu majeraha yetu ya kisiasa na kijamii, Muswada huu utayawekea chumvi na kuyafanya yawe makubwa zaidi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment