10 October 2013

WAKAMATWA NA ATM 243 ZA BENKI YA NMB



  Na Faida Muyomba, Geita

 Jeshi la Polisi mkoani Geita,limefanikiwa kuwakamata watu wawili wakiwa na kadi 243 za watu mbalimbali wilayani Chato, zinazotumika kutolea fedha kwenye ATM za Benki ya NMB kinyume cha sheria.


Kamanda wa polisi mkoani Geita, Leonard Paulo,aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake,kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7, usiku katika Kijiji cha Kitela wilayani Chato.

  Aliwataja watuhumiwa hao kuwani Gidion Matiku (22) na Seleman Hassan(30) mkazi wa Chato wote wakiwa wafanyabiashara wa duka la nafaka pamoja na vifaa vya ujenzi.

“Tunawashikilia watu hawa tukiendelea kufanya uchunguzi zaidi kwa nini wanamiliki hizi kadi zote za ATM zilizotolewa na Benki ya NMB wanazifanyia nini kwa sababu zina majina ya wateja mbalimbali, ambao ndio wamiliki halali wanaotambuliwa na benki hii na si wao,” alisema Kamanda huyo.

  Alisema, kuwa kitendo hicho cha kumiliki kadi hizo za benki,ni kinyume cha sheria na kuwa jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi zaidi ambapo pindi ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara moja.

  Katika hatua nyingine,jeshi hilo linawashikilia watu wawili wakazi wa kijiji cha Runzewe wilayani Chato,wakituhumiwa kutaka kumuua kwa kumkata mapanga mkazi mmoja wa kijiji hicho kwa kinachodhaniwa ni ugomvi wa shamba.

  Kamanda wa polisi mkoani Geita,Leonard Paulo,aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bw.Marco Mathias (46) na Bw.Boniphace Shija (33) wote wakazi wa kijiji hicho na kuwa tukio hilo lilitokea juzi.

No comments:

Post a Comment