22 October 2013

TANZANIA YAPAA KIUCHUMI EAC



 Na Penina Malundo
  Imeelezwa kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri kiuchumi katika nchi za Afrika Mashariki ukilinganisha na Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi
. Akitoa takwimu hizo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Morrice Oyuke wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa robo ya Pili ya Mwaka 2013, alisema Tanzania inashikilia nafasi ya pili.
  Oyuke alisema kuwa, moja ya Sababu inayofanya uchumi wa nchi kukua kulinganisha na nchi nyingine ni pamoja na Serikali kuongeza nguvu katika kuwekeza ukuaji wa shughuli za uchumi wa kilimo nchini.
 “Serikali inatumia Sera zake katika kukuza uchumi wa nchi, kwa kutumia sekta yenye watu wengi, kama ya kilimo, kwani asilimia kubwa ya wananchi wanawekeza katika kilimo huku mvua nazo zimekuwa za kutosha katika mikoa inayozalisha mazao mengi na kufanya wakulima kuwa na mazao mengi ya biashara pamoja na ya chakula,” alisema Oyuke.
  Alisema kuwa, katika nchi za Afrika Mashariki nchi inayoongoza katika ukubwa wa uchumi ni Kenya ikifuatiwa na Tanzania hivyo uzalishaji hapa nchini umekua kwa kiasi kikubwa kuliko nchi ya Uganda, Rwanda pamoja na Burundi.
 “Sisi ni wa pili katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa nchi zote za Afrika Mashariki ikiongozwa na nchi ya Rwanda na kwa ukubwa wa uchumi wa nchi. Kenya inaongoza tukifuatiwa na sisi, Uganda, Rwanda pamoja na Burundi,” alisema Oyuke.
  Aliongeza kuwa Pato la Taifa limeweza kuongezeka kwa robo ya pili ya mwaka 2013 kutoka asilimia 6.4 kwa robo ya mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 6.7 kwa mwaka huu.
  Alisema kuwa, ukuaji wa pato la taifa unatokana na uboreshwaji wa sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya kilimo, uvuvi, viwanda, ujenzi pamoja na nishati.

No comments:

Post a Comment