24 October 2013

RIPOTI : UHALIFU WAONGEZEKA TANZANIA Na Grace Ndossa
  Hali ya ulinzi na usalama nchini, imeendelea kudorora kutokana na ongezeko la matukio ya uhalifu yanayoendelea kufanywa na baadhi ya watu. Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Kupunguza Umaskini nchini (REPOA), Dkt. Abel Kinyondo, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akiwasilisha taarifa ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Afrobarometa, kuhusu matukio ya uhalifu nchini.

Alisema utafiti huo umefanyika kwa miaka tisa 2003-2012, ambapo matukio ya uhalifu yamekuwa yakiongezeka kila siku kuanzia mwaka 2008-2012 pamoja na ukosefu wa vituo vya polisi katika baadhi ya maeneo. Aliongeza kuwa, utafiti huo umebaini kuwa wananchi wengi hawaripoti matukio ya uhalifu polisi kutokana urasimu mkubwa uliopo, hivyo wananchi hawasilikizwi pamoja na polisi kudai rushwa.
"Utafiti huu ulikuwa ukiangalia ongezeko la vitendo vya uhalifu nchini tangu mwaka 2008-2012, miaka ya nyuma matukio ya uhalifu yalikuwa machache sana," alisema Dkt. Kinyondo.Alisema utafiti huo kwa Tanzania umefanyika Mei na Juni 2012 na ulikusanya maoni ya watu 2,400 kila Mkoa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Profesa Samwel Wangwe, alisema utafiti huu umefanywa na nchi 34 ambapo kwa Tanzania inaongoza kuwa na hofu ya uhalifu asilimia 40."Nchi inayofuata kwa kuwa na hofu ya vitendo vya uhalifu ni Afrika Kusini (asilimia 38), Cameroon (37), Liberia (35), na Swaziland asilimia 34," alisema.
  Aliongeza kuwa, utafiti uliofanyika mwaka 2011-2012 ni asilimia 42 tu ya watu walioripoti matukio ya uhalifu polisi nchini Tanzania ambapo idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na nchi ya Nigeria ambayo nusu ya wananchi wake wanaripoti taarifa mbalimbali polisi.Prof. Wangwe alisema Jeshi la Polisi nchini linapaswa kushirikiana na wananchi ili kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo ili waweze kukamatwa.
  Aliitaka Serikali ishirikiane na sekta binafsi ili kujenga vituo vya polisi na kununua vitendeakazi.
Ofisa Mnadhimu wa Jeshi la Polisi, Beatus Silla, alikubaliana na utafiti huo juu ya upungufu wa vituo vya polisi na kusisitiza kuwa, suala la ulinzi na usalama ni la watu wote, si polisi pekee kwani jeshi hilo halina polisi wa kutosha.
"Kutokana na uhaba wa vituo vya polisi, tumelazimika kuweka Inspekta wa Polisi kila tarafa na wamepewa pikipiki za kufanyia kazi ili kupunguza vitendo vya uhalifu," alisema.
  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi na Utawala, Profesa Amon Chaligha, alisema wananchi wanapaswa kushirikiana na vyombo vya ulinzi ili kuimarisha utawala bora.
Alisema utafiti huo pia unaonesha wanawake wanaogopa zaidi kuliko wanaume kutokana na jeshi hilo kutumia mabomu katika mikutano mbalimbali hivyo kuwafanya waogope.

No comments:

Post a Comment