04 October 2013

NDEGE YAANGUKA DAR Na Goodluck Hongo
  Watu wawili wamenusurika kufa baada ya ndege ndogo aina ya Cessna 204, 5H-IBB, kuanguka jana asubuhi katika eneo la Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Gongolamboto, Dar es Salaam.

Ndege hiyo ilipata hitilafu kwenye injini ikiwa angani na watu wawili ambao ni rubani wa ndege hiyo, Aziz Salim (59), mkazi wa Upanga aliyekuwa akimfundisha rubani mwanafunzi anayeitwa Ahmed Mahmud (24), raia wa Kenya, mkazi wa Kariakoo.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, ACP Hamisi Selemani, alisema watu hao walijeruhiwa baada ya ndege hiyo kuanguka.
"Rubani wa ndege hii (Salim), ambayo inamilikiwa na Kampuni ya As Salaam, alitoa taarifa kuhusu hitilafu ya injini akiwa angani na kusema muda wowote ndege inaweza kuanguka hivyo aliamua kuishusha eneo ambalo halina makazi ya watu na kuharibika vibaya," alisema Kamanda Selemani.
Aliongeza kuwa, ndege hiyo iling'oka tairi la mbele, kuharibika mabawa yake pamoja na kubondeka ambapo majeruhi hao walipata majeraha maeneo ya usoni na maeneo mengine ya miili yao. Alisema majeruhi hao walikimbizwa Hospitali ya Jeshi Gongolamboto na baadaye kuruhusiwa.

No comments:

Post a Comment