04 October 2013

MEYA ILALA AMLIPUA MAHANGA

Dkt. Makongoro Mahanga

Na Heri Shaaban

  Baraza la Madiwani Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, limelaani vikali migogoro ya kisiasa isiyo na tija kwa wananchi hasa barua iliyoandikwa na Mbunge wa Segerea, Dkt. Makongoro Mahanga ambayo ilishikiwa bango na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia.


Barua hiyo inadaiwa kusababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bw. Gabriel Fuime, kusimamishwa kazi bila kufuatwa taratibu za utumishi hivyo kutia doa utumishi wake wa muda mrefu.

Meya wa manispaa hiyo, Bw. Jerry Silaa, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kikao cha Baraza la Madiwani na kusisitiza kuwa, Dkt. Mahanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, hakujali msaada wa Bw. Fuime ambaye aliutoa jimboni kwake Katika Uchaguzi Mkuu 2010.

Inadaiwa kuwa, kuna barua ya siri iliyoandikwa kwenda TAMISEMI ikimtuhumu Bw. Fuime na Bw. Silaa wakidaiwa kuhusika na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu.

Kutokana na tuhuma hizo, Bw. Fuime alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake ambapo miongoni mwa tuhuma hizo ni kushindwa kusimamia mapato ya halmashauri hiyo na ukodishaji unaotia shaka katika Soko la Samaki Feri.

  Hata hivyo, Bw. Fuime anadaiwa kukanusha madai ya kusimamishwa kazi bali aliamriwa na TAMISEMI apumzike kwa madai ofisi hiyo imepokea tuhuma dhidi yake.

  Katika hatua nyingine, Bw. Silaa alisema manispaa hiyo inatumia sh. milioni 10 ambazo ni gharama za simu kwa mwezi ambazo kwa mwaka ni sh. milioni 12. Gharama nyingine ni safari za ndani na nje sh. milioni 50 kwa mwezi (kwa mwaka milioni 600).

  Wakati huo huo, madiwani wa manispaa hiyo wamemchagua Bw. Kheri Kessy kuendelea na wadhifa wake wa Naibu Meya wa Manispaa hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.

  Bw. Silaa aliwapongeza madiwani kwa uamuzi huo na kudai kuwa, Bw. Kessy ni kiongozi shupavu ambaye amempa msaada mkubwa na kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati za Kudumu waliochaguliwa na kuwataka waongoze kamati hizo kwa moyo na uadilifu.

No comments:

Post a Comment