07 October 2013

MAENDELEO HAYATALETWI NA MIJADALA ISIYOISHA-KIKWETENa Eckland Mwaffisi
   Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala isiyoisha na vikao vya kulipana posho bali kwa viongozi kufanya maamuzi na kuyatekeleza haraka.Alisema Tanzania inachelewa kupata maendeleo ya haraka kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kuanza kujadili badala ya kuchukua maamuzi na kuyatekeleza.

Rais Kikwete alimetoa tahadhari hiyo ya kuchelewesha maendeleo wakati akizindua Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani.Akizungumza na wananchi kabla ya kuzindua kambi hiyo na kukagua shughuli zinazofanywa na vijana 50 kutoka vijiji vya Wilaya ya Rufiji ambao wanajifunza mbinu na maarifa ya kilimo bora katika kambi hiyo, alitaka kujua kama kampuni mbili zilizoomba ardhi ya kulima kisasa katika Bonde la Mto Rufiji, zimepewa ardhi ya kuanza kulima.
Awali katika maelezo yaliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja, yaliashiria kuonesha kampuni hizo Frontline Development Partners na Lukurilo Holdings Company Limited, yalipewa ardhi na Mamlaka hiyo kama yalivyokuwa yameomba.
  Pamoja na maelezo hayo, Rais Kikwete alipotaka kujua kampuni hizo zilipewa ardhi kiasi gani Bw. Masanja alisema Frontline Development Partners walioomba hekta 20,000 lakini walikuwa hawajapewa hata moja na Lukurilo Holdings walioomba hekta 12,000 na kupewa 4,000 tu.
  Rais Kikwete alishangazwa na hali hiyo na kusema; "Kwa miaka minne sasa, tunazungumza jambo hili bila kufikia uamuzi wake, tumewahi kujadili suala hili pale Ikulu, Dar es Salaam na kukubaliana, nini kimetokea.
  "Tulikubaliana kutekeleza jambo hilo sasa tunaendelea kujadili nini, nchi yetu itachelewa sana kupata maendeleo kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kuanza kujadili," alisema.
  Aliongeza kuwa, Tanzania haiwezi kuendelea kwa mijadala na vikao vya kulipana posho visivyoisha kwani Frontline Company imeanza kuomba ardhi ya kulima miaka mitano iliyopita.
  Aliwataka viongozi wote wanaohusika na suala hilo kukutana wiki ijayo na kusisitiza kuwa, nchi inakwamishwa na watu wa namna hiyo.
  Mapema Rais Kikwete amewaambia viongozi wa kambi hiyo ambayo inamilikiwa na RUBADA kuwa, kazi ya kambi hiyo iwe kuandaa vijana wa kujiajiri kwa kilimo cha kisasa si kuandaa watu wa kutafuta kazi ya kuajiriwa katika kilimo.
"Tunaandaa wakulima wazuri, vijana si kuandaa kundi la watu wa kutafuta ajira ya kilimo, hatuwezi kuwa na kambi ya namna hii ikiandaa kundi la watu wa kutafuta ajira, kijijini utaajiriwa na nani kama siyo kushiriki kilimo," alihoji Rais Kikwete.
  Alisema amefurahishwa na uamuzi wa kuandaa vijana hao ili waweze kushiriki katika kilimo kwa sababu mageuzi ya kilimo yataletwa na vijana. Rais Kikwete alizindua mradi mkubwa wa maji Mjini Kibiti na kukabidhiwa boti ambazo zitafanya shughuli za kubeba wagonjwa katika maeneo ya Nyamisati na visiwa vya jirani.

No comments:

Post a Comment