11 October 2013

MAADHIMISHO YA MTOTO WA KIKE KUFANYIKA LEO Na Mwandishi Wetu
  Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe , leo anatarajiwa kuwa miongoni mwa washiriki wa mjadala mpana kuhusu njia za kumaliza tatizo la ndoa za utotoni , ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya mtoto wa kike Duniani.

Mjadala huo umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA), Kikundi cha Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania yanayoshughulikia jinsia, kwa kushirikiana na Jukwaa la Graca Machel linalopigania hadhi ya mtoto.
Maadhimisho ya pili ya siku ya mtoto wa kike duniani nchini Tanzania yenye kauli mbiu kuwa; "Kuwawezesha wasichana, kuhakikisha haki zao za binadamu na kushughulikia ubaguzi na unyanyasaji wao ni muhimu kwa maendeleo ya familia nzima ya wanadamu."
Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya ndoa za utotoni duniani. Kwa wastani, watoto wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.
Mjadala huu unalenga kuchochea zaidi ushirikiano ulioundwa kwa ajili ya matokeo bora kwa watoto ikiwa ni pamoja na wasichana na wavulana na hasa uraghibishi endelevu na wa kina kuhusu suala la ndoa za utotoni na ajenda pana kuhusu haki za wanawake na watoto.
Washiriki wengine ni pamoja na Shekhe Alhad Musa Salim, Askofu Jacob ole Paul Mameo, Mkurugenzi Mtendaji wa KIWOHEDE, Justa Mwaituka na Bi.Valerie Msoka , Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania atakayeongoza mjadala huo na Jama Gulaid ambaye ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini.
Mama Graca Machel atawasalimia washiriki kwa njia ya video, washiriki wote watakuwa na nafasi ya kuuliza maswali jopo la wazungumzaji na pia kushiriki mjadala kwa kuchangia mada kwa kutumia utaalamu na ufahamu.
Wakati huo huo ,Grace Ndossa,anaripoti kuwa Shirika la Kimataifa la Plan International, leo linaadhimisha siku hiyo kwa kuelimisha jamii na kutetea haki za mtoto wa kike.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaama jana kuhusu kampeni hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa Plan International, Jorgen Haldorsen, alisema kampeni hiyo itafanyika katika viwanja vya Shule ya Benjamini Mkapa.
Alisema lengo ni kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana milioni nne duniani na zaidi ya wasichana 300,000 nchini Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga shuleni, kupata stadi za kiufundi na maisha pamoja na kujikimu.
  Alisema pia kuwawezesha wasichana kushiriki katika shughuli mbalimbali katika jamii na kulindwa kwa kukabiliana na vikwazo dhidi ya maendeleo ya mtoto wa kike.
  Alisema inanuia kuongeza stadi, maarifa na uelewa wa hatari zinazowakabili watoto wa kike kutokana na ukatili wa kijinsia katika familia, shuleni na jamii katika maeneo mbalimbali.
  Aliongeza kuwa Plan inatambua kuwa ubaguzi dhidi ya wasichana ni sababu kuu inayosababisha umaskini miongoni mwa watoto, wasichana kwa wavulana.
  Alisema wasichana wana uwezekano mkubwa wa kukosa chakula , wanakabiliwa zaidi na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na wanategemewa kufanya kazi nyingi za nyumbani na hivyo kuwafanya wasifikie upeo na uwezo wao wa kiakili.
  Alisema kwa hapa Tanzania kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi na shirika hilo Oktoba mwaka jana kwa kushirikiana na wizara mbalimbali za Serikali, mashirika ya haki na ustawi wa watoto, mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, mashirika ya kitaifa na kimataifa, watoto pamoja na wadau wengine.
  Alisema kwa mwaka huu siku hiyo inasherehekewa kupitia shughuli na matukio mbalimbali nchi nzima ambayo yanajumuisha watoto na jamii zao, vitengo na wizara mbalimbali na taasisi wabia za kijamii.

No comments:

Post a Comment