23 October 2013

KIVUMBI CHA LIGI KUU KUENDELEA LEO  •   YANGA HUKU SIMBA KULE

Na Neema Ndugulile
  Ligi Kuu ya Vodacom, inatarajia kutimua vumbi tena leo katika viwanja vitatu tofauti, ambapo Yanga itaikaribisha Rhino Rangers katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga itaingia uwanjani hapo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bila kutarajiwa dhidi ya watani wao wa jadi, Simba katika mechi iliyopigwa Jumapili kwenye uwanja huo na kulazimishwa sare ya mabao 3-3.
Katika mechi hiyo Yanga, ilijiamini kuifunga Simba baada ya kuwa inaongoza mabao 3-0 hadi mapumziko, lakini kipindi cha pili kibao kiligeuka na mabao yote kurudishwa.
  Hivyo katika mechi ya leo, Yanga ambayo ipo nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, itataka kutoka na ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wake.
  Wakati Yanga wakiwa Uwanja wa Taifa, watani wao Simba watakuwa wageni wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
  Mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi, Dominic Namisanya kutokana Dodoma, inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na historia ya timu hizo.
  Simba itaingia uwanjani ikiwa ya tatu katika msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 19, huku Coastal Union wapo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 11.
  Nayo Tanzania Prisons ambayo imepoteza mechi mbili zilizopita ugenini dhidi ya Ashanti United na Simba, itarejea kwenye uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine kwa kuikaribisha Kagera Sugar.
  Katika hatua nyingine, mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea leo kwa mechi moja ya kundi A, itakayozikutanisha Tessema na Villa Squad katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment