07 October 2013

KESI TOZO LAINI ZA SIMU KUSIKILIZWA LEONa Rehema Mohamed
  Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajiwa kuanza kusikiliza kesi ya kupinga tozo ya sh. 1,000 kwa kila laini ya simu iliyofunguliwa na Taasisi ya Watumiaji Bidhaa na Huduma nchini.Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na jopo la Majaji watatu ambao ni Lawrence Kaduri, Aloysius Mujuluzi na Salvatory Bongole, iliyofunguliwa chini ya hati ya dharula.

Katika kesi hiyo, walalamikaji wanaiomba mahakama hiyo itangaze kuwa, sheria iliyopitishwa na Bunge inayotaka kila mtumiaji wa simu ya mkononi kukatwa sh. 1,000 kila mwezi kwa kila laini ni kandamizi.
Taasisi hiyo ilidai kuwa, watumiaji wengi wa simu za mkononi hawana uwezo wa kukatwa fedha hiyo kwa mwezi na kusisitiza itawaathiri watumiaji wa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa madai ya walalamikaji, sheria hiyo inakiuka matakwa ya katiba ya nchi ya uhuru wa kupashana habari na kuiomba mahakama kuifuta sheria hiyo wakidai ni kandamizi.
Mawakili wa walalamikaji kutoka Kampuni ya uwakili ya Rex, Lugano Mwandamo na Merkizedeki Lutema, walidai wateja wao wanataka mahakama imzuie Waziri wa Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA), kutotoza kodi hiyo hadi maombi yao yatakapotolewa uamuzi.Katika kesi hiyo, upande wa serikali uliwakilishwa na wakili Kelley Mwitasi.

No comments:

Post a Comment