21 October 2013

CHADEMA WAMLIPUA SITTA

  • WADAI AMESHINDWA KUJENGA BARABARA URAMBO


Na Goodluck Hongo, Urambo
 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kama kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi mwaka 2015, watabadilisha matumizi ya Ofisi ya Spika iliyojengwa na mbunge wa Urambo Mashariki, Bw. Samuel Sitta.

 Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara wilayani humo, mkoani Tabora, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa, alisema ofisi hiyo wataibadilisha kuwa wodi ya wazazi ili iweze kuwasaidia wanawake wanaoteseka kupata huduma ya afya.
   Alisema Bw. Sitta alijenga jengo hilo ili litumike kama ofisi ya Spika wa Bunge kabla ya kumaliza muda wake wakati mji huo hauna barabara za lami wala hospitali za kutosha hivyo kama watapewa ridhaa, watalibadili matumizi yake.
   Alisema Mkoa huo una historia kubwa nchini lakini hauna maendeleo ambapo badala ya Serikali kujenga barabara nzuri na kuwapa wananchi maji safi na salama, Bw. Sitta alijenga ofisi akiamini hata ondoka katika kiti hicho.
  "Sitta amekuwa mbunge tangu 1976 katika jimbo hili lakini hadi leo hakuna barabara za lami mjini wala zinazoingia na kutoka katika jimbo hili," alisema Mtemelwa..Aliongeza kuwa, miaka ambayo Bw. Sitta amekuwa mbunge wa jimbo hilo inamtosha hivyo ni lazima wananchi wachague mbunge kutoka upinzani ambaye hataogopa kusema ukweli ili kuharakisha maendeleo yanayohitajika.
  Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi inayoundwa na Mikoa ya Katavi,Tabora na Kigoma, Bw. Shabani Mambo, alisema kwa muda mrefu wakazi wa Kigoma walikuwa wakikichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini walikosa maendeleo na baada ya kuchagua upinzani, hivi sasa Kigoma imebadilika kwa kiasi kikubwa.
  Alisema lazima wananchi wawe na upeo wa kufikiria kwani Mkoa wa Tabora wenye majimbo tisa, hakuna hata moja ambalo limechukuliwa na upinzani na matokeo yake hakuna maendeleo..Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kubadili uongozi uliopo kwani licha ya Mkoa huo kubarikiwa Mawaziri, hadi leo hauna maendeleo ya kujivunia

No comments:

Post a Comment