03 October 2013

ICC YAAGIZA RAIA WA KENYA AKAMATWE




THE HAGUE, Uholanzi
   Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), imetoa kibali cha kukamatwa raia Mkenya, Bw. Walter Osapiri Barasa ambaye anatuhumiwa kujaribu kuwahonga mashahidi ili wajiondoe katika kesi inayomkabili Makamu wa Rais nchini Kenya, Bw. William Ruto.

   Viongozi wa mashtaka katika mahakama hiyo, walisema mtuhumiwa huyo ameshtakiwa kwa makosa matatu likiwemo la kutumia njia za ufisadi kumshawishi shahidi mmoja na mkewe kwa kumlipa sh. milioni 1.4 za Kenya au dola za Marekani 16,200, ili wajiondoe kama mashahidi.
   Kiongozi wa mashtaka, Fatou Bensouda, alisema ana ushahidi wa kutosha unaoonesha njama za Bw. Barasa kutaka kuwahonga mashahidi ili wajiondoe katika kesi dhidi ya Bw. Ruto.
   Bensouda alisema, kuna mtandao wa watu wanaofanya kila wawezalo ili kuporomosha kesi hilo ambapo Bw. Barasa aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kuwa yupo tayari kujitetea mbele ya mahakama hiyo kwani hana hatia.
  Bw. Ruto na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, wameshtakiwa kwa kupanga na kuongoza ghasia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 ambapo watu 1,200 walifariki dunia.
  Wakati huohuo , ICC imelazimika kuwa na vikao virefu zaidi vya kusikiliza kesi dhidi ya Bw. Ruto kwa sababu ya muda uliopotea kutokana na mshtakiwa huyo kurejea Kenya kwa dharura.
  Jaji anayeongoza kesi hiyo, Chile Eboe-Osuji, alisema mahakama itaangalia uwezekano wa kusikiliza kesi wiki ijayo siku ambayo wangepumzika ili kuruhusu kesi nyingine kusikilizwa.
  “Kama tunavyojua, sote tumepoteza muda katika kesi hii kwa sababu ya matukio ambayo hayakuweza kuepukika,” alisema. Kesi dhidi ya Bw. Ruto iliahirishwa Septemba 23, mwaka huu, kutokana na shambulizi la kigaidi katika jengo la kibiashara la
  Westgate, Mjini Nairobi, nchini Kenya Septemba 21, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 60. Hata hivyo Jaji Eboe-Osuji alisisitiza kuwa, kesi hiyo itaahirishwa kwa muda ili kutoa nafasi ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya Rais Kenyatta, Novemba 12, mwaka huu ambaye ni mshtakiwa mwenza na Bw. Ruto.


No comments:

Post a Comment