Na Rehema
Mohamed
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
imetoa amri ya kukamatwa wadhamini wawili waliowadhamini raia wawili wa
Pakistan waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kukutwa na dawa za kelevya kinyume
cha sheria ili waitwe mahakamani na wajieleze baada ya washtakiwa waliomdhamini
kukimbia.
Wadhamini hao ni Amiral Sharif, mkazi
wa Kisutu na Elias Kumrudin, mjumbe wa nyumba 10 Mtaa wa Libya
.Wengine ni Mohamed Bahishi, mkazi wa
Chang'ombe, Dar es Salaam na Nazar Mohamed Nuru, mkazi wa Mtaa wa Libya, Kisutu,
Dar es Salaam, ambao ni waajiriwa wa kampuni ya Songea Mining &
Construction Ltd Holdings.
Amri hiyo ilitolewa jana mahakamani
hapo na Jaji Grace Mwakipesile, baada ya washtakiwa hao na wadhamini wao,
kutokutokea mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi yao.Mahakama hiyo pia imetoa hati ya
kuwakamata washtakiwa hao, ili kufikishwa mahakamani kuendelea na kesi
inayowakabili.
Washtakiwa waliokimbia ni Abdul Ghan
Bux na Shahbaz Malik, pamoja na Watanzania wawili Fredy William Chande na Kambi
Seif ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kuingiza dawa za kulevya
nchini kinyume cha Sheria ya Kuzuia Usafirishaji na Biashara ya Dawa za
Kulevya.
Katika kesi hiyo namba moja ya mwaka
2012, washtakiwa hao wanadaiwa kuingiza nchini dawa hizo aina ya heroin ambazo
zinadaiwa kuwa na thamani ya sh. bilioni 6.Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza
kusikilizwa jana hatua ya awali ambapo washtakiwa hao wangesomewa maelezo ya
awali juu ya mashtaka yanayowakabili, lakini ilikwama kusikilizwa baada ya
washtakiwa wawili (Wapakstani) kutokomea kusikojulikana.
Kutokana na hali hiyo, Wakili wa
Serikali Theophil Mutakyawa, alidai kesi ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa
awali lakini aliiomba mahakama itoe amri ya kukamatwa washtakiwa na wadhamini
wao kwa kutofika mahakamani.Alidai kumbukumbu zinaonesha Julai,
2011, washtakiwa wote walipewa dhamana na mahakama hiyo hivyo mshtakiwa wa tatu
na nne, wamekiuka masharti ya dhamana kutokufika mahakamani.
"Katika mazingira haya ni rai ya
Jamhuri kwamba itolewe hati ya kuwakamata washtakiwa namba tatu na nne ili
waweze kufika kwa tarehe itakayopangwa, pia itolewe hati ya wito wa mahakama
kwa wadhamini wao waje wajieleze," alidai Mutakyawa.
Jaji Mwakipesile, alipomuuliza Wakili
wa washtakiwa hao, Yassin Membar, alijibu hana taarifa zozote za washtakiwa hao
hivyo alikubaliana na maombi ya Jamhuri kuamuru washtakiwa hao wakamatwe na
samansi kwa wadhamini wao kama upande wa mashtaka ulivyoomba.Kesi hiyo iliahirishwa hadi tarehe
nyingine itakayopangwa na Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu.
Washtakiwa hao wanadaiwa kwa nyakati
tofauti kati ya Januari mosi na Februari 21, 2011 katika maeneo tofauti nchini
na Pakistani, walikula njama na kutenda makosa ya kusafirisha, kuingiza nchini
dawa za kulevya.Inadaiwa walikamatwa Februari 21, 2011,
Mtaa wa Jongoo eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam, wakiwa na dawa hizo zenye
uzito wa gramu 179,000 zenye thamani ya sh. bilioni 6.2.
Wakati kesi yao hiyo ikiendelea katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika hatua za awali, washtakiwa hao
waliwasilisha Mahakama Kuu, Dar es Salaam, maombi ya dhamana.Wakati maombi hayo yakisikilizwa,
upande wa utetezi ulidai hakuna uthibitisho wa thamani ya pesa za dawa hizo
kwani hakuna hati inayothibitsha thamani hiyo.
Mawakili wa utetezi walidai hata hati
ya mashtaka haielezi ni nani aliyetuma dawa hizo kutoka Pakistan na
aliyezipokea nchini.Waliongeza kuwa, hati ya mashtaka
haikueleza taarifa binafsi za washtakiwa kama umri na utaifa wao hivyo kutokana
na dosari hizo washtakiwa wana haki ya kupewa dhamana.
Baada
ya kusikiliza hoja za pande zote, Julai 6, 2011, Jaji Upendo Msuya aliwapa
dhamana, akisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha sababu za kuwanyima
dhamana baada ya ukikiri kutowasilisha nyaraka muhimu za kutetea hoja zao.
Hawa kwanini walipewa dhamana? Taifa linataka majibu toka mahakamani waliotoa hiyo dhamana, tukumbuke kuna wanachi hawapewi dhamana je hawa pk walipata vipi dhamana na hali ni wageni? Ina maana hapa kuna mchezo mchafu ambao mahakama inauelewa
ReplyDelete