11 September 2013

RUFAA YA 'WAZIRI' DAFTARI LEO



 Na Rachel Balama
MAHAKAMA y a Rufaa Tanzania leo itaanza kusikiliza rufaa ya kesi ya Naibu Waziri wa zamani wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dkt.Maua Daftari, dhidi ya mfanyabiashara Fatuma Salimini Said.

Dkt. Daftari ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM, alikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwamuru kumlipa mfanyabiashara huyo sh. milioni 100.7.
Rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, linaloongozwa na Jaji Januari Msoffe, akisaidiana na Jaji Dkt. Steven Bwana na Jaji Sauda Mjasiri.
Rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa leo chini ya jopo jipya la majaji watatu wa Mahakama hiyo ambapo wakili wa mkata rufaa (Dkt. Daftari) atawasilisha hoja zake za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, kabla ya mawakili wa mjibu rufaa kujibu hoja hizo.
Awali rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa Juni 12, 2013 na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Nathali Kimaro, akisaidiana na Jaji Salum Massati na Jaji William Mandia, lakini ilikwama kusikilizwa baada ya Jaji Kimaro kujiondoa.
Jaji Kimaro alitangaza kujitoa katika rufaa hiyo baada ya kubaini kuwa alishawahi kuisikiliza kesi ya msingi mwaka 2011, akiwa Mahakama Kuu.
Katika kesi ya msingi, mlalamikaji Fatuma Salimin Said, alikuwa akimlalamikia Dkt. Daftari kumtapeli fedha taslimu pamoja na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 200.
Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Fatma alikuwa akimdai Dkt. Daftari sh. milioni 100,092,400 alizompa ili amnunulie vifaa mbalimbali kati ya mwaka 1994 na 1997, lakini mlalamikiwa hakufanya hivyo

1 comment:

  1. Kesi hii wangeimaliza weneywe tu bila kupelekana mahakamani,

    ReplyDelete