20 August 2013

WANANCHI WAHIMIZWA KUCHANGIA CHAKULA SHULENI


  Na Eliasa Ally, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christina Ishengoma amewataka wazazi mkoani humo kuchangia chakula shule za msingi na za sekondari za kata hiyo ili wanafunzi waweze kupata mlo wa mchana wakati wakiwa shuleni badala ya kurudi nyumbani ili kuongeza kiwango cha ufaulu
.Akizungumza jana ofisini kwake kuhusiana na uchangiaji wa chakula shuleni, Dkt. Ishengoma alisema kuwa wazazi wa watoto ambao wanasoma katika shule za msingi na sekondari katika mkoa huo wamekuwa nyuma katika kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi waweze angalau kupata mlo mmoja wa mchana hali ambayo imesababisha baadhi ya wanafunzi ambao wanashinda njaa kushindwa kuyapokea vema masomo wanayofundishwa.
"Natoa wito kwa wananchi wote kuhakikisha kuwa mpango huu unafanyika katika shule zetu zote mkoani Iringa ili kuongeza kiwango cha ufaulu cha wanafunzi pamoja na kuimarisha afya zao, ninawaomba viongozi wa vijiji na serikali za mitaa wahamasishe na kusimamia vizuri ili kuhakikisha kuwa mpango huu unakuwa endelevu," alisisitiza Dkt. Ishengoma.
Hata hivyo, alizitaja shule za msingi zilizopo mkoani Iringa ambazo wanafunzi wake wanapata chakula na wasiopata chakula kuwa katika Manispaa ya Iringa Mjini jumla ya shule 49 zilizopo, zinazopata chakula zipo 21, Iringa Vijijini shule zipo 145 zinazopata chakula zipo 129
Pia wilaya ya Kilolo zipo shule 111 zinazopata chakula zipo 98 na Mufindi kuna shule za msingi 176 ambapo zinazopata chakula zipo 72 na kufanya jumla ya shule za msingi 320 mkoani Iringa kupata chakula cha mchana ambapo 481 wanafunzi wake hawapati chakula cha mchana.
Akizungumzia shule za sekondari katika Mkoa wa Iringa, Dkt. Ishengoma alizitaja zinapata chakula katika Manispaa ya Iringa zinazopata chakula zipo 11 kati ya sekondari 26, Iringa Vijijini zipo sekondari 32 zinazotoa chakula zipo 21, wilaya ya Kilolo kuna sekondari 38 zinazotoa chakula zipo zipo 19 ambapo Mufindi kuna sekondari 55 zinazotoa chakula zipo 36; na hivyo kufanya jula ya sekondari 87 zinazotoa chakula kati ya sekondari 151 zilizopo.
Aidha, Mkuu wa mkoa alizitaja changamoto nyingine ambazo zinaukabili Mkoa wa Iringa kuwa ni pamoja na kutokuwepo kwa maji safi kwa matumizi ya wanafunzi katika maeneo ya shule, uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa mpango wa chakula shuleni.
Nyingine ni ushiriki mdogo wa wananchi katika kuchangia chakula, ukosefu wa wafadhili, mabweni, miundombinu katika shule husika yakiwemo mabwalo ya chakula pamoja na vifaa vya kuchukulia chakula na kuhifadhia

No comments:

Post a Comment