15 August 2013

UZALISHAJI SARUJI KUONGEZEKA NCHINI- TCCL



 Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Saruji Tanga (TCCL) na TDI imezindua ujenzi wa uchimbaji msingi kwa ajili ya kupanua kiwanda hicho mkoani Tanga ili kuongeza uzalishaji wa saruji awamu ya pili tani 775,000 kwa mwaka. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ambao ulifanyika jana kiwandani hapo eneo la Pongwe mkoani humo, Mwenyekiti wa Bodi ya TCCL, Lau Masha alisema awamu ya kwanza ya upanuzi wa kiwanda ilifanyika mwaka 2009-2010 na awamu hii ya pili itakamilika mwaka 2015. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya dola la kimarekani milioni 165 hadi kukamilika.

"Ndipo, tuliposimika mtambo wa pili wa kusaga saruji, mashine ya kupakia saruji ambavyo kwa pamoja viliongeza uwezo wa kusaga saruji kwa asilimia 73, kufikia tani milioni 1.3 kwa mwaka," alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi.
Alisema, uwezo wa uzalishaji clinker ulibakia tani laki tano kwa mwaka, hivyo kuwalazimu kuziba uwiano huo wa clinker na saruji kwa kuagiza clinker kutoka nje. "Kama mnavyojua bidhaa hii (clinker) kutoka nje inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwepo kuyumba kwa thamani ya fedha za kigeni, mfumuko wa bei na uharamia katika eneo la Ghuba.
"Mradi huu umekuwa kwenye maandalizi kwa muda mrefu, hivyo tunayo furaha kubwa kwamba leo (jana) tunazindua uanzilishi wa ujenzi wake," aliongeza Mwenyekiti huyo. Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa 'kiln' mpya, pamoja na 'crusher' eneo la kuchanganyia malighafi, mtambo wa kusaga udongo na mkaa.
"Gharama za mradi huu unakisiwa kuwa dola za kimarekani milioni 165 na ujenzi wake unategemewa kumalizika kwenye robo ya kwanza ya mwaka 2015. "Bodi yetu ina imani kwamba wahusika na wadau wote wa mradi huu watatekeleza wajibu wao kikamilifu, kuhakikisha kumalizika kwa ujenzi wa mradi huu kwa muda uliopangwa," alisema.
Mbali na kuongeza uwezo wa kuzalisha clinker ili kuendana na uwezo wa kusaga saruji alisema mradi huo pia utasaidia kupunguza gharama za uzalishaji, pia utaongeza ubora na wingi wa saruji hapa nchini. "Mradi huu unadhihirisha imani waliyo nayo wawekezaji kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika juhudi zake za kuhakikisha utulivu na amani nchini, pamoja na mazingira bora ya kibiashara.
"Kama kawaida yetu kwa miaka mingi, Tanga Cement (Kampuni ya Saruji Tanga) itaendelea na juhudi zake za kuendeleza huduma kwa jamii, ikilenga katika nyanja za afya, elimu, mazingira na maendeleo ya jamii," aliongeza Mwenyekiti huyo wa Bodi.
Awali Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa, mwaka jana kampuni yake ilitumia zaidi ya sh. milioni 400 kwenye huduma za kijamii ambapo kati ya hizo asilimia 37 ilikuwa kwa Mkoa wa Tanga peke yake.

No comments:

Post a Comment