- JWTZ WATHIBITISHA
Na Rehema Mohamed
JESHI la Ulinzi
la Wananchi wa Ta n z a n i a ( JWT Z ) , limethibitisha kuuawa kwa wanajeshi
saba na wengine 14 kujeruhiwa vibaya akiwemo askari polisi mmoja wote kutoka
Tanzania baada ya kushambuliwa na waasi.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa jeshi hilo nchini, Kanali
Kapambala Mgawe, alisema wanajeshi hao ni miongoni mwa askari wanaolinda amani
kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN), Mjini Darfur, nchini Sudan.
Alisema wanajeshi
hao waliuawa katika shambulio la kushtukiza ambalo lilifanywa na waasi hao
Julai 13, mwaka huu, saa 3 asubuhi, wakati wakiwasindikiza waangalizi wa amani
kutoka Khor Abeche kwenda Nyara mjini humo
.
Shambulio hilo lilitokea umbali wa
kilomita 20 kutoka Makao Makuu ya Kikosi hicho ambapo miongoni mwa
waliojeruhiwa ni pamoja na Maofisa na askari kutoka mataifa mengine.
Aliongeza kuwa, wakati kikosi cha
wanajeshi wa Tanzania kikishambuliwa, kilikuwa na askari 36 lakini hakuwa
tayari kutaja majina ya wanajeshi waliouawa.
"Hatuwezi kutaja majina ya wanajeshi
waliouawa kwani ni mapema mno, tusubiri taratibu nyingine za kijeshi
zikamilike, kwa sasa mazingira ya ulinzi Mjini Darfur, yanafanyika kwenye
daraja sita ambayo si ya kutumia silaha.
"Kutokana na shambulio hili,
tunafanya mawasiliano na UN waruhusu matumizi ya daraja la saba ili kuongeza
uwezo zaidi wa kujilinda na mashambulizi pale askari wanaposhambuliwa na
waasi," alisema Kanali Mgawe.
Alisema vifo hivyo vimeisikitisha JWTZ
kwani tukio hilo limetokea katika mazingira ya ulinzi wa amani ambao hauna
matumizi ya silaha.
"Hii ni taarifa ya awali juu ya tukio
hili...baada ya tukio hili kikosi chetu Mjini Darfur kilitoa taarifa Makao
Makuu Dar es Salaam, miili ya marehemu na majeruhi iliondolewa eneo la tukio na
kupelekwa Nyara ambako kuna Hospitali Kuu ya eneo la operesheni kwa taratibu za
matibabu," alisema.
Kanali Mgawe alisema, JWTZ linawasiliana
na familia za marehemu juu ya taratibu za mazishi pamoja na UN kuhusu taratibu
zote muhimu zinazohusiana na matibabu ya wanajeshi waliojeruhiwa katika eneo la
tukio.
Katika hatua nyingine, Kanali Mgawe
alisema tayari ujumbe maalumu umeteuliwa kwenda Khartom, Darfur kuzungumza na
mamlaka husika kuhusu shambulizi hilo.
Jumla
ya askari 875 wa jeshi hilo waliondoka nchini Februari mwaka huu kwenda Sudan
ili kulinda amani chini ya Mpango wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment