02 April 2013

Ngawaiya kuwaburuza Diwani, Ofisa mtendaji mahakamani


Na Gladness Mboma

MDHAMINI wa Taasisi ya Maendeleo Tarafa ya Kibosho (KIDEFU)mkoani Kilimanjaro,Bw.Thomas Ngawaiya ametishia kuwafikisha mahakamani Diwani wa Kata ya Kirima,Bw.Paul Kileo na Ofisa Mtendaji Kata ya Kibosho, Bw.Gilbart Nyamsha kwa kutangaza kuuza mapipa ya lami yenye thamani ya shilingi bilioni 2.


Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Dar es Salaam, Bw.Ngawaiya alisema kuwa viongozi hao walitoa tangazo la kuuzwa kwa lami hizo ambazo zimenunuliwa kutokana na michango ya wananchi wa Kibosho kwa ajili ya kutengeneza barabara za lami kwa kata 28 za wilaya hiyo ya Kibosho.

"Nilishangaa kusikia kwamba viongozi hawa wawili wamekaa vikao na vijiji viwili na kushauriana kuuza lami ambayo hawajui ni ya nani na kisha wakaanza kutoa matangazo watu wajitokeze kununua

"Cha kusikitisha zaidi ni kwamba maamuzi haya wameamua kuchukua wao wenyewe bila ya kumshirikisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na badala yake wamewapelekea nakala ya tangazo la kuuza lami hiyo,"alisema Ngawaiya.

Alisema kuwa mapipa ya lami ambayo yaliifadhiwa kiwanja cha ofisi ya Kirima Boro KNCU katika kijiji cha Kirima kati kata ya Kirima yeye ndiye aliyepewa kazi ya kusimamia ujenzi huo wa barabara.

Bw. Ngawaiya alisema kuwa zaidi ya mapipa 3000 waliyapeleka, ambapo mapipa 50 yaliibiwa baada ya kumvunja miguu Bw. Alex Mushi ambaye alikuwa mlinzi wa mali hiyo.

Alisema kuwa watendaji hao wasidhani kwamba lami hiyo imewekwa kama pambo, kwani kuna makubaliano ya pamoja kati ya serikali na mfuko kuangalia namna gani ya kutumia lami hiyo hata kama imeharibika.

Bw. Ngawaiya alisema kuwa lami hiyo inayotengenezwa kwa vijiji 28 katu hatokubali kuona inauzwa na watu wachache wenye uchu na uroho wa kutumia vibaya mali za umma na kusisitiza kuwafikisha mahakamani.

"Nina mkataba na serikali juu ya kujenga barabara ya lami ya kibosho na mikataba hiyo imeiniwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Ujenzi Jonh Magufuli,"alisema.

Alisema kuwa wasione barabara za Kibosho zinajengwa kuna mikataba na mawasiliano na kuwataka kuacha kukurupuka na kuwataka wasichezee mali za serikali kwa sababu ni faida kwa serikali na vizazi vijavyo.

Bw. Ngawaiya alisema kuwa mapipa kumi ya lami iliyoibiwa ni lazima watendaji hao wahilipe na kusisitiza kwamba wao wanajua ni nani aliyeiba.

Alisema kuwa mtu yoyote atakayebainika kuiba mapipa hayo ya lami watafanyiwa kitu kibaya ili iwe fundisho kwa watu wengine na kusisitiza kwamba kesi atakazo fungua ni mbili.

Bw. Ngawaiya alisema kuwa wamefungua kesi polisi mbili ambazo ni jalada MS/RB/13529/12-10/2012 na MOS RB/16148/2012 na kwamba amekwishawasiliana na wakili wa kesi zote na zitakwenda kwa pamoja.No comments:

Post a Comment