02 April 2013

Kuanguka ghorofa neema kwa madereva


Na Mwandishi Wetu

KIFUSI cha ghorofa 16 ambalo lilidondoka mwishoni mwa wiki katika Mtaa wa Indira Ghandi, Barabara ya Bagamoyo, Dar es Salaam, kimekuwa biashara nzuri katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo ambapo baadhi ya watu hukununua sh. 40,000 hadi 70,000 kwa roli
moja kutokana na ujazo wake.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika eneo la Jangwani, umebaini kuwa, baadhi ya madereva wa magari yanayozoa kifusi hicho, ndio wahusika wa biashara hiyo.

Akizungumza na mwandishi wetu, mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Bw. Mohamed, alisema tangu ghorofa hilo lianguke, biashara hiyo ya kununua kifusi imeshika kasi wengi wao wakiitaji nondo.

“Siku ya kwanza kutokea tukio hili, kifusi kilikuwa kikiuzwa sh.
40,000 lakini kazi ya uokoaji ilivyokuwa inaendelea, bei hiyo ilikuwa ikiongezeka na kufikia sh. 70,000 kwa roli moja lenye
nondo nyingi.

“Mimi nimenunu bifusi vitatu kwa sh. 40,000 vilivyokuwa na mawe na kokoto kiasi, jirani yangu alinunua kwa sh. 70,00 ambacho kilikuwa na idadi kubwa ya nondo,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi hao walilalamikia unene wa nondo hizo na kuhoji kwanini mkandarasi alizitumia katika ujenzi wa ghorofa ambao unahitaji nondo kubwa.

Uchunguzi huo umebaini kuwa, tangu kuanguka kwa jengo hilo, baadhi ya wakazi wa Jangwani wamefungua viwanda vidogo vya kunyoosha na kukata nondo usiku na mchana ili kwenda kuziuza.

Biashara hiyo imeonekana kuwanufaisha madereva wa malori yanayosomba vifusi hivyo kwa kujiongezea kipato.

No comments:

Post a Comment