04 March 2013

Kagasheki, Meya 'waipasua' CCM *Mgogoro wao wadaiwa kuvuka mipaka *Nape: Tume iundwe kuchunguzi tuhumaNa Theonestina Juma, Bukoba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kimesema mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, kati ya Meya wa Manipaa hiyo Dkt. Anatory Amani na mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kashakeki, umevuka mpaka.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimemuomba Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), kuunda tume ili kuchunguza tuhuma
zinazoelekezwa kwa Dkt. Amani.

Katibu NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Bw. Nape Nnauye, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini humo akiwa safarini kurejea Dar
es Salaam, baada ya kufanya ziara ya siku moja mjini humo.

Bw. Nnauye alisikitishwa na mgogoro huo kuendelea ndani ya Manispaa hiyo na kusababisha baadhi ya madiwani kusisua vikao
hivyo kuathiri utendaji kazi wa shughuli za maendeleo.

Alisema upo umuhimu wa Serikali kuu kuingilia kati mgogoro
huo ambapo katika mazungumzo na madiwani hao, waliwaomba
watekeleze wajibu wao wa kushiriki vikao.

“CCM Taifa imesikitishwa na mgogoro huu ambao hauna tija kwa yeyote, chama au wananchi...kuna tuhuma nyingi kwa Dkt. Amani kuhusu ujenzio wa soko, Kituo cha Mabasi, viwanja na uendeshaji halmashauri hivyo tume ikija, itachunguza na kutoa taarifa ambayo tutaiweka hadharani kwa sababu maneno hayo yametoka ndani na sasa yako nje hivyo ni vyema wananchi wakajua,” alisema.

Aliongeza kuwa, tume hiyo ina mamlaka ya kuwasimamisha uongozi baadhi ya watu ili kupista uchunguzi lakini wao
wataangalia sheria zinasemaje.

Akizungumzia athari za mgogoro huo, Bw. Nnauye alisema ni pamoja na kusababisha mgawanyiko ndani ya chama hasa kwa
madiwani na kuathiri utekelezaji wa ilani ya CCM kwani bajeti isipopitishwa, pesa hazitatoka kwa wakati hivyo miradi mingi itakwama kuanza kutekelezwa.

“Waathirika wakubwa watakuwa wananchi kwa kukosa huduma muhimu kama maji, dawa na elimu ndio maana nasema inahitajika nguvu kubwa kuumaliza mgogoro huu.

“Tumeigawa jamii kutokana na mgogoro huu, kundi moja linapita upende mwingine na  kuzomeana, tukiendelea hivi hali itakuwa mbaya zaidi na kupoteza sifa ya mji huu,” alisema.

Alisema wakati mgogoro huo unaanza, si kweli kwamba CCM kilikaa kimya bali kuna hatua zilichukuliwa na si kila mgogoro unapoanza lazima chama hicho Taifa kiingilie kati bali ngazi
ya chini inaposhindwa ndio huingilia.

No comments:

Post a Comment