11 February 2013

Zitto apinga kuvunjwa POAC *Adai ni kinyume cha katiba, sheria ya ukaguzi


Na Mwandishi Wetu

SIKU mbili baada ya Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, kutangaza babadiliko ya Kamati za Kudumu za Bunge kabla
ya kuahirisha mkutano wa 10 mjini Dodoma huku akiifuta
Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), uamuzi
huo umepingwa vikali na aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati
hiyo Bw. Kabwe Zitto (CHADEMA).


Alisema uamuzi wa Bi. Makinda kuifuta kamati hiyo ni kinyume
cha katiba ya nchi, Sheria ya Ukaguzi wa Umma inayotaja kamati tatu za Bunge kusimamia fedha za umma na unarudisha nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji.

Bw. Zitto aliyasema hayo katika taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari kulalamikia uamuzi huo na kusisitiza kuwa,
lazima Bi. Makinda adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi
hiyo hawaka iwezekanavyo.

Alisema Bi. Makinda amedhihirisha jinsi anavyotoa maamuzi
yake bila kuzingatia masilahi ya nchi wala uwajibikaji nchini
badala yake amekuwa akibeba hoja za Serikali na kujenga
Bunge kibogoyo wakati jukumu lake ni kusimamia vikao.

“Lazima Spika afahamu kuwa, mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge hivyo lazima adhibitiwe vinginevyo nchi itaumia.


“Maamuzi haya yameleta sintofahamu kwa wananchi wengi, wafuatiliaji wa masuala ya Bunge na uwajibikaji katika nchi
hivyo ni muhimu tufahamu uundwaji wa POAC ulitokana na
misingi gani,” alisema Bw. Kabwe.

Aliongeza kuwa, kufutwa kwa kamati hiyo kunarudisha nyuma maendeleo makubwa ya kujenga Bunge imara lenye meno hivyo
yanapaswa kupingwa na kiola mdau wa uwajibikaji nchini.

Alisema baada ya Tanzania kuingia katika mchakato wa ubinafsishaji, mashirika mengi ya umma yaliuzwa na mengine
kufa wakati huo kukiwa na chombo kusimamia uendeshaji wa mashirika ya umma (SCOPO).

Bw. Kabwe alisema, Bunge lilikuwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ambayo ilifutwa mwaka 1997 kutokana
na hatua za ubinafsishaji.

“Ni wazi kuwa wakati huo Mashirika ya Umma hayatakuwapo
hivyo kukukuwa na haja ya kuwepo kamati hii lakini mwaka 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alifanya mkutano wa Uwajibikaji na kueleza kuwa, mashirika haya bado yapo na kwa kuwa hesabu zao haziangaliwi, fedha nyingi za
umma zinapotea,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa CAG, alisema Katiba ya nchi ibara ya 143(5) inamtaka atoe taarifa za ukaguzi za mashirika hayo hivyo
aliliomba Bunge liunde kamati ya POAC ili iweze kupokea, kujadili na kutoa maelekezo kuhusu mahesabu ya mashirika na kusimamia ufanisi wake.

“Pia alishauri kamati ya POAC isimamie sera ya ubinafsishaji wa mashirika husika ambapo Spika wa Bunge wakati huo, aliiunda kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge za mwaka 2007.

“POAC iliundwa rasmi Februari 2008 na mimi kupewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza...sababu za kuwepo kamati hii bado zipo na zina maana sana kuliko ilivyokuwa kabla,” alisema.

Aliongeza kuwa, majukumu ya POAC ni kushughulikia mahesabu yaliyokaguliwa ya mashirika hayo, kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma, kutathmini ufanisi wa mashirika husika na kufuatilia utekelezwaji wa sera ya
ubinafsishaji wa mashirika.

Kuanzia mwaka 2008, CAG amekuwa akitoa taarifa za mahesabu
ya mashirika hayo kama Katiba ya nchi inavyomtaka na sheria ya ukaguzi ya mwaka 2008 ambapo POAC inatakiwa kuwasilisha bungeni taarifa ya mwaka ya mahesabu ya mashirika hayo.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na uwazi kuliko
kamati nyingine zote za Bunge.

Bw. Kabwe alisema taarifa ya mwisho waliitoa katika mkutano
wa saba wa Bunge Aprili 2012 na kusababisha kutolewa hoja ya  kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo iliyosababisha mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.

Hatua hiyo ni muhimu sana ili kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini lakini wakati kamati hiyo ikijiandaa na taarifa
ya mwaka 2012, katika mkutano wa Bunge la 11, Spika ameivunja kamati hiyo.

“Magizo ya mwisho ya POAC yalizuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa mikopo kwa Serikali bila kuwepo mikataba, hivi sasa Serikali imekopa zaidi ya sh. trilioni 1.2 kutoka mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya miradi mbalimbali.

“Mikopo hii ya fedha za wafanyakazi haina mikataba yeyote hivyo  POAC iliona jambo hili ni hatari kwani fedha za wafanyakazi zitapotea na kuleta madhara kwa wastaafu nchini,” alisema.

Alisema katika maelezo yake wakati akiifuta kamati hiyo, Bi. Makinda alisema nchi nyingine duniani hazina kamati kama ya POAC, jambo ambalo Bw. Kabwe alidai halina ukweli wowote.

Aliongeza kuwa, waliomshauri Bi. Makinda walimdanganya
bali nchi zote za Afrika Mashariki zina Kamati ya kusimamia
Mashirika ya Umma.

Alisema kimsingi kamati hiyo ilipaswa kuongezewa nguvu ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye kampuni binafsi kama
BP (kwa sasa Puma), Kilombero Sugar na nyinginezo badala
ya kuifuta.

Katika uamuzi wake, Bi. Makinda alisema hivi sasa kazi za POAC zinafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), itakayoendelea na jukumu la kuchangua taarifa za CAG na Serikali Kuu.

Kamati nyingine iliyofutwa ni ya sheria ndogo, kuunda kamati
mpya tatu na nyingine kuzifanyia marekebisho ikiwa ni hatua
ya kuimarisha usimamizi wa Bunge kwa shughuli za Serikali.

1 comment:

  1. SI UONGO UMEKUWA UKITUMIA JUKUMU HILO KUFANYA KAMPENI ZA URAIS KWA KUTOA TAARIFA ZA UKAGUZI KWENYE VYOMBO VYA HABARI HATA KABLA YA KUJADILIWA BUNGENI

    ReplyDelete