07 February 2013

Wanawake wapewa mbinu ya kupambana na unyanyasaji


Na Charles Lucas

UMOJA wa Wanawake Wafanyabiashara wa Soko la Ilala wameipongeza Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Equality For Growth (EFG) kwa kuwaelimisha kuhusu mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Wakizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali waliotembelea soko hilo Dar es Salaam juzi, wanawake hao wamesema vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake vilivyokuwa vimekithiri vimeanza kupungua kwenye soko lao kutokana na elimu waliyoipata kupiti kauli mbiu ya 'Nipe riziki Usinipe matusi' inayoendeshwa na taasisi hiyo.

Akizungumza wakati wa tathimini ya mpango huo mhamasishaji wa umoja huo, Bi.Consolata Mwita alisema awali soko hilo lilitawaliwa na ubabe kwa wanaume kuwanyanyasa wanawake wakati wa kazi ikiwamo kuwatukana matusi ya nguoni au kuwapiga bila kuchukuliwa kwa hatua dhidi yao.

Pia vitendo vya kuwakopa biashara zao na kukaidi kulipa ni kero nyingine iliyokuwa imeshamiri na kufikia hatua ya kukata tamaa ya kuendelea na biashara kwenye soko hilo.

"Siku moja mwenzetu alifanyiwa unyanyasaji kwa kuvuliwa nguo wakati akidai fedha zake' kitendo ambacho ni udharirishaji usiovumilika, ambap unapaswa kukemewa kwa nguvu zote, " alisema.

Hata hivyo wananchi wanawake hao wamelalamikia kutozwa ushuru wa sh. 1000 kila siku kwa biashara ya mboga za majani na kusababisha kushindwa kulipa kwa wakati.

Akijibu kuhusu malalamiko hayo makamu mwenyekiti wa kamati ya soko hilo, Bw.Said Kisoma alisema ni kweli vitendo vya unyanyasaji vipo lakini uongozi wa soko umechukua hatua za kudhibiti tabia hiyo ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa na kuwapa adhabu za faini za papo kwa hapo ili kuondokana na kero hiyo.

Pia alikiri kushirikiana na EFG katika harakati za kupambana na vitendo hivyo katika maeneo yote ya soko na kuongeza kuwa tabia hiyo imepungua kutokana na elimu inayoendelea kutolewa na taasisi hiyo kwa wafanyabiashara wote.

Kuhusu malalamiko ya ushuru mkubwa alisema suala hilo linashughulikiwa katika ngazi ya manispaa kutokana utaratibu huo kuwapo kabla ya kamati mpya kuchaguliwa mwishoni mwa mwaka jana hivyo baada ya kafanyiwa kazi taarifa itatolewa bila kificho.

Taasisi ya EFG inatoa elimu ya kupambana na kero mbalimbali kwa wanawake katika maeneo ya kazi na imeanzia kwenye masoko ya Kinondoni na Ilala lengio likiwa ni elimu hiyo kutolewa nchini kote.

No comments:

Post a Comment