27 February 2013
Wagombea urais Kenya wachuana katika mdahalo
NAIROBI, Kenya
SUALA la uchumi, ardhi na wakimbizi limechukua nafasi kubwa katika mdahalo wa mwisho wa urais nchini Kenya uliofanyika juzi nchini humo ukiwashirikisha wagombea wanane.
Mdahalo huo ambao ulirushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio nchini humo, ulianza kuzungumzia mkakati
wa kila mgombea katika kushughulikia suala la uchumi pamoja
na matumizi ya fedha za umma.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Bw. Raila Odinga, ambaye ni mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama cha ODM na Muungano wa Cord, alisema;
“Hivi sasa, matumizi ya Serikali yako juu sana hivyo tutapendekeza viwango vya miashahara kwa viongozi vipunguzwe pamoja na mimi mwenyewe ili niweze kuwa kiongozi wa mfano,” alisema.
Mdahalo huo, pia ulizungumzia tatizo la umiliki wa ardhi ambalo limedumu muda mrefu tangu nchi hiyo ipate uhuru wake kutoka
kwa Waingereza.
“Baada ya uhuru, tatizo la umiliki wa ardhi halikushughulikiwa ambapo watu wa Pwani walinyanyaswa zaidi na Serikali tatu zilizopita...hati za umiliki wa ardhi zilitolewa kwa watu
kutoka bara badala ya wenyeji,” alisema Paul Muite
kutoka Chama cha Safina.
Suala hilo lilijadiliwa kwa kina huku baadhi ya wagombea wakimpaka matope mpinzani wao Naibu Waziri Mkuu, Bw. Uhuru Kenyatta, wakidai hawezi kushughulikia suala hilo kikamilifu kama atachaguliwa katika nafasi ya urais kwa madai yeye mwenyewe anamiliki maeneo makubwa ya ardhi.
“Kwa mfano, rafiki yangu Uhuru Kenyatta, familia yake inamiliki maeneo makubwa ya ardhi hapa Kenya,” alisema Martha Karua, mgombea mwanamke pekee wa kiti hicho.
Akijitetea kuhusu tuhuma hizo, Bw. Kenyatta alisema yeye na familia yake hawakupata ardhi mahali popote kinyume na sheria isipokuwa kwa kununua kutoka kwa wauzaji wa hiari na
wameitumia ardhi hiyo kuimarisha uchumi.
Kwa mujibu wa Sauti ya Ujerumani (DW), hadi sasa kuna wakimbizi wa ndani kutokana na ghasia zilizotokana na
Uchaguzi Mkuu wa 2007 ambao hawajapewa makazi.
Wagombea hao walipata wakati mgumu kueleza watakavyotatua tatizo hilo ambalo limechangiwa na ukosefu wa ardhi.
“Ningependa kuona hatuna wakimbizi wa ndani kwa sababu ya siasa...shida iliyotokea ni pesa zilizotengwa, wale wenye mashamba makubwa wanayauza kwa bei kubwa ambayo Serikali inashindwa kuimudu kwa kuyanunua,” alisema Musalia Mudavadi ambaye
ni mgombea wa Chama cha Muungano wa Amani.
Mambo yote yaliyojadiliwa yametokana na maswali ambayo yaliwasilishwa kwa waandalizi wa mdahalo ambapo kila
mgombea alipata nafasi sawa ya kuuza sera zake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment