27 February 2013

Mbaroni kwa wizi wa mil. 20/- ATM *Wakutwa kwenye mashine na kadi 150 *Mmoja anamiliki ofisi ya mikopo Tukuyu


Na Rashid Mkwinda, Rungwe

JESHI la Polisi Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, linawashikilia watu wanne kwa kosa la kukutwa wakitoa fedha kwenye mashine
ya (ATM), inayomilikiwa na Benki ya NMB, mjini Tukuyu.

Watu hao walikutwa na kadi 150 za watu tofauti pamoja fedha
taslimu zaidi ya sh. milioni 20 walizotoa katika mashine ya
ATM, iliyopo karibu na Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya.

Habari zilizolifikia gazeti hili, zinasema wahusika wa wizi huo wamefahamika kwa majina ya Bw. Miraji Kipale (34), Bw. Joseph Peter (20) na Bw. Juma Kabero (20), wote wakazi wa Tukuyu.

Mwingine ni Bw. Jumanne Mgere (29), ambaye ni mkazi wa
Mbozi, ambao kati kadi walizokamatwa nazo, 136 tayari
walizitumia kuchukua fedha katika ATM.

Habari zaidi zinazongeza kuwa, Bw. Kipale anamiliki ofisi ambayo inaitwa “Nyarusi”, ambayo imekuwa ikitoa mikopo ya fedha kwa watu mbalimbali wakiwemo watumishi wa Serikali hasa walimu
na kurudisha mkopo kwa riba.

Baadhi ya wakopaji, wanadaiwa kuweka bondi vitu mbalimbali
vya thamani pamoja na kadi zao za benki (ATM). Watuhumiwa
hao pia walikutwa na orodha na majina ya watu 150 pamoja
na namba zao za ATM.

Baada ya tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Chrispin Meela, alitoa tamko la kusitisha huduma za utoaji mikopo kwa watu wote wanofanya biashara hiyo.

Alisema halmashauri hiyo itaitisha mkutano wa wafanyakazi wote wa wakiwemo walimu ili kuwahadharisha juu ya mikopo ambayo inatolewa na watu mbalimbali wilayani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Diwani Athumani, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao na kuongeza kuwa, jeshi hilo litatoa taarifa rasmi leo kuhusiana na wizi huo.

No comments:

Post a Comment