12 February 2013

Ucheleweshaji fedha za miradi wakwamisha maendeleo


Na Pendo Mtibuche,Dodoma

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kondoa imesema kuwa  inakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na kuchelewa  kupokelewa kwa fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati.


Hadi kufikia Desema 2012 ni kiasi cha asilimia 11 tu ya fedha za miradi ya maendeleo ndizo zilizokuwa zimepokelewa.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Bw.Isdory Mwalongo  wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa changamoto nyingine ambayo imekuwa ikiwakabili kwa muda sasa ni pamoja na ile ya mapato ya ndani yanaashiria kutofikiwa  kutokana na baadhi ya mawakala kuanza kushindwa kuwasilisha fedha za makusanyo mbali na mikataba  iliyofikiwa hivyo kuifanya halmashauri kufikia hatua ya kuvunja mikataba.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa ili kuboresha mapato katika halmashauri hiyo ipo mikakati mbalimbali ambayo imebainishwa ikiwemo ya kuongeza usimamizi wa ushuru wa mazao, kutangaza utalii wa ndani,kutunga sheria ndogo ndogo za kukusanya  fedha kutoka katika viwanda na leseni ya makazi.

Kwa upande wake naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Kondoa, Bw.Hamisi Mwenda aliwaonya watumishi wa halmashauri hiyo kuacha tabia ya kufanya kazi kwa fitina na majungu na kuleta migawanyiko ndani ya halmashauri.

Alisema kuwa hivi sasa amebaini tatizo la baadhi ya wakuu wa idara kufanyakazi kwa kuzungukana jambo ambalo alisema kuwa halmashauri hiyo imeanza kuchukua hatua na yeyote atakayebainika kufanya kazi kwa mtindo huo atachukuliwa hatua kali.

No comments:

Post a Comment