12 February 2013

TFDA Arusha yateketeza bidhaa za milioni saba


Na Queen Lema,Arusha

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), imeteketeza tani moja na robo ya shehena ya bidhaa mbalimbali zenye thamani ya sh.milioni saba ambazo zimekwisha muda wake wa matumizi na nyingine hazijasajiliwa na pia hazionyeshi muda wake wa matumizi kumalizika.


Akizungumza jana katika zoezi hilo la kuteketeza bidhaa hizo kwenye jalala kuu lililopo eneo la Muriet katika halmashauri ya Jiji la Arusha,meneja wa kanda ya Kaskazini, wa TFDA,Damas Matiko, alisema bidhaa hizo zimekamatwa katika msako uliofanyika ndani ya wiki moja kutoka maduka ya vyakula na super market.

Alizitaja bidhaa hizo zilizoteketezwa kuwa ni  mafuta ya vyakula,juisi,soda za kopo aina ya Pepsi, majani ya chai,dawa za miswaki za kichina, sukari, maji ya chupa,unga wa maziwa wa uji wa watoto uliopo kwenye makopo,vinywaji vikali.

Matiko alisema kuwa bidhaa hizo hazikidhi viwango vinavyotakiwa na hazijasajiliwa na Shirika la Viwango nchini (TBS),na zingine zimeandikwa lugha isiyofahamika ,zingine zimeghushiwa tarehe ya mwisho ya kutumika, hivyo zina madhara makubwa kwa watumiaji na pia hazimhakikishii usalama mlaji.

Alisema zoezi hilo la kukamata bidhaa hizo bandia limefanyika kuanzia Februari 4- 8 mwaka huu ,ambapo mamlaka hiyo imelazimika kuendesha msako huo kwenye maduka baada ya kubaini kuwepo kwa bidhaa zisizokuwa na kuathiri afya za walaji.

Aliongeza kuwa zoezi hilo ni endelevu lengo ni kuhakikisha bidhaa zisizokuwa na viwango zinatokomezwa katika maduka yote ili kulinda afya za walaji .

Matiko alitoa wito kwa wananchi wanaonunua bidhaa zao kwenye maduka makubwa ya kuuza vyakula,'Super market', kusoma maelezo ya bidhaa wanazonunua ili waelewe muda wa matumizi badala ya kununua kwa haraka na kwenda kutumia wakati mwingine wanaweza kununua bidhaa ambazo muda wake umeshakwisha na zikawa ni madhara kwao.

"Wananchi wawapo na mashaka na bidhaa hizo zilizoko kwenye maduka zikiwemo ambazo lugha na maelezo yake hayaeleweki watoe taarifa TFDA, au idara ya afya halmashauri ya jiji la Arusha,lengo ni kulinda afya za walaji," alisisitiza Matiko.

Aliyataja baadhi ya madhara hayo kuwa ni pamoja na kupata magonjwa kama vile saratani,kuharisha maumivu ya tumbo,kupata mzio unaotokana na kula vyakula vya aina fulani, wengine hunenepa na kuwa na miili mikubwa mfano kwa wanawake.

Kwa upande wake kaimu afisa afya mkuu wa jiji la Arusha, Alan Sumari, amewataka wafanyabiashara kuingiza nchini bidhaa zenye viwango ili kuepuka hasara ya bidhaa hizo kuteketezwa na TFDA.

No comments:

Post a Comment