26 February 2013

Tusimtoe kafara Dkt.Kawambwa, elimu inahitaji maamuzi ya kitaifa


Na Joseph Edward

TANGU yatangazwe matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambayo wanafunzi wamefali kwa kiwango kikubwa kumeibuka mjadala hasa kwenye vyombo vya habari ndani na nje ya nchi.


Kila mmoja amekuwa akizungumza lake kuhusiana na matoke hayo kwa lengo la kuonesha kuguswa kwake na hali hiyo. Karibu kila kona mjadala ndiyo huo hadi imefikia hatua hata mambo mengine muhimu katika taifa letu yamesahaulika.

Hiyo inaonesha ni kwa jinsi gani Watanzania wanavyogusa na elimu. Lakini mijadala kama hii haikuanza leo.

Kwa wale wenye kumbukumbu watakubaliana na mimi kwamba kwa takribani miaka miwili kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau wa elimu kuhusiana na kushuka kwa ubora wa elimu na pamoja na  ufaulu.

Pia matokeo ya mwaka 2012 ya Kidato cha Nne yaliyotangazwa  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt.Shukuru Kawambwa, yameongeza hasira za Watanzania hadi kufikia hatua wengi wanataka ajiuzulu.

Malalamiko haya ni ya msingi ni vizuri wadau wa elimu wakatafakari kwa kujiuliza swali moja.Swali hilo ni je  kuachia ngazi kwa Waziri Kawambwa ndiyo litakuwa jawabu la watoto wetu kufaulu na hatimaye kuongeza ubora wa elimu nchini.

Ifike wakati Watanzania tukubaliane kuwa ubora wa elimu haupimwi kwa ufaulu wa mitihani peke yake, bali yapo mambo mengi muhimu yanayotakiwa kuangaliwa ili kupima ubora wa elimu ambayo ni pamoja na kuwepo kwa walimu ubora, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia na umahiri wa wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu.

Ninayataja haya ili kuonesha jinsi kuondoka kwa Dkt. Kawambawa katika Wizara ya Elimu kusivyoweza kumaliza  changamoto zilizopo za kuwafanya walimu wetu wawe mahiri, yaani walimu wanaosomea ualimu wawe wale waliofaulu Daraja  la Kwanza na la Pili katika mitihani ya Kidato cha Nne au cha Sita, kupatikana kwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuboresha mazingira ya shule.

Lazima Watanzania wakubaliane kuwa uamuzi wa kupanga na kuweka vipaumbe vya Taifa si wa Dkt.Kawambwa peke yake, ni wa Watanzania wote ni muhimu tukaamua kuipa kipaumbele sekta ya elimu na Walimu kwa ujumla kwa kutenga bajeti ya elimu ya kutosha ili walimu walipwe vizuri na hivyo kusababisha wanafunzi wanaofaulu katika madaraja ya juu kuchagua kusomea ualimu.

Ningeunga mkono kujiuzulu kwa Dkt.Kawambwa kama ningeambiwa kuwa amepewa bajeti ya kutosha kuboresha elimu lakini ameshindwa kuitumia au imetumika vibaya kinyume na ilivyopitishwa Bungeni.

Taarifa za kuaminika kutoka wizarani zinasema kuwa katika bajeti ya Wizara anayoiongoza Waziri Kawambwa asilimia 85 inatengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini na asilimia 15 inayobaki ndiyo inayotakiwa kutumika katika elimu ya awali, Msingi, Sekondari, ukaguzi wa shule, Elimu ya Ualimu, Elimu ya Ufundi na Elimu ya Juu.

Kwa bajeti hii anatakiwa apatikane waziri atakayetumia  miujiza kufanikisha malengo yanayotakiwa katika elimu. Kinachotakiwa tufanye ni uamuzi muhimu kama Watanzania kwa ujumla wa kutenga bajeti ya kutosha kuhudumia walimu na sekta ya elimu kwa ujumla badala ya kumsakama Dkt.Kawambwa.

Bado Watanzania tunashindwa kufanya maamuzi magumu katika kupanga vipaumbele vyetu kwani utasikia kuwa hatuwezi kuwaongezea mishahara walimu kwa kuwa walimu hao ni watumishi wa umma kama walivyo watumishi wengine.

Katika nchi zilizoendelea mwalimu analipwa mshahara wa juu kuliko watumishi wengine na ndiyo maana wanaosomea ualimu wanakuwa ni wale waliofaulu vizuri zaidi katika mitihani yao.

Lakini hapa Tanzania mwalimu akihitimu chuo kikuu na kipangiwa kituo cha kazi mfano mikoa ya Mtwara na Lindi anaenda kuishi kwenye nyumba ya makuti. Hii nini kwa sababu Serikali imeshindwa kuwajengea walimu nyumba.

Sasa hapa ni nani wa kulaumiwa ni Dkt.Kawambwa au Serikali nzima. Shule zingine hazina walimu huku zingine zikifundishwa na mwalimu mmoja,lakini lawama hii pia inaelekezwa kwa Waziri Kawambwa, huku ni kumtoa kafara.

Tujiulize mazingira hayo ndiko kumthamini mwalimu ili aweze kunoa akili za wataalamu wa baadaye katika Taifa. Uamuzi kama huu haufanywi na Waziri wa Elimu peke yake, unahitaji maamuzi ya Kitaifa.

Tukirejea kwenye matokeo ya Kidato cha Nne na kuangalia sababu ambazo zimekuwa zikitolewa kwanini wanafunzi wamefeli: Kwanza inachukuliwa kama ni tatizo la shule za wananchi (Kata) kwa kisingizio tu kwamba hazina vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kuwa na miundombinu mibovu na kukosa maabara na walimu wa kutosha.

Ni lazima tujiulize shule za Kata zilianza lini na wakati huo ufaulu ulikuwaje? Je, Dkt.Kawambwa anayepigiwa kelele za kujiuzulu ni yeye aliyeanzisha shule hizi au yalikuwa ni maamuzi yetu ya kitaifa?

Tuliamua wenyewe wananchi kuzijenga shule hizi na ndiyo maana zinaitwa shule za sekondari za wananchi na uamuzi huu ulikuwa na nia ya kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na elimu ya sekondari nchini ili hatimaye kuongeza idadi ya wataalamu watakaohitimu elimu ya juu.

Utekelezaji wa uamuzi huu ulianza tangu Awamu ya Tatu ya Uongozi wa Taifa letu na kuendelezwa kwa kasi zaidi katika Awamu ya Nne hasa chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu aliyejizuru, Edward Lowassa.

Ongezeko la shule na idadi ya wanafunzi wa sekondari limeibua changamoto mbalimbali ambazo ni lazima tukabiliane nazo hasa kuhusu ubora wa Elimu inayotolewa. Ni lazima tuongeze walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na kuboresha mazingira ya shule zetu.

Kazi ya kusomesha walimu haiwezi kukamilishwa kwa mwaka mmoja au miwili, inahitaji muda na rasilimali za kutosha. Hivyo tujitahidi kama Taifa ili hatimaye tupate walimu wa kutosha na hasa walimu wa Sayansi na Hisabati. 

Hata hivyo ni vyema tukaangalia ni kwanini ufaulu wanafunzi unashuka sasa, tukianza na wanafunzi wenyewe ambao wanaonesha wamepoteza shauku na morali ya kusoma kwa bidii na badala yake wanatumia muda mwingi kuchezea simu na mitandao ya kijamii ambayo imekuwa ikiwapotezea muda.

Mara ngapi tumewaona wanafunzi wakiwa vituoni, ama kwenye mitaa wakirandaranda wakati wa vipindi. Wanafunzi wa sasa hawana muda wa kujisomea jioni. Televisheni na mitandao imekuwa ndiyo masomo ya kujisomea jioni.

Zamani mwalimu alikuwa anafundisha asilimia 20 halafu mwanafunzi inabidi utafute asilimia 80, kwa siku hizi wanafunzi wanapenda mteremko ndiyo maana kila kitu wanamwachia  mwalimu, yaani wameshindwa tu kumbeba mwalimu siku ya mtihani awajibie  maswali wanabaki kukamatwa na vibuti.

Tuwaangalie wazazi wa sasa je, ni wale wazazi waliokuwa na muda wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao ya shule. Wengi wao wamekuwa wakiwapa watoto wao malezi ya kuwadekeza na hivyo kutowafundisha stadi za maisha na umuhimu wa kujituma katika elimu, na zaidi wakijali miradi na kazi zao kuliko hata kufuatilia watoto wao.

Mara ngapi wazazi na watoto wanaishi nyumba moja lakini hawaonani kwa mwezi mzima? Leo hii mwalimu akijitahidi kumpa mwanafunzi malezi inakuwa ni kesi kubwa baina ya mzazi na mwalimu na hata wazazi wakiitwa kwenye vikao vya shule ni wazazi wangapi wanahudhuria vikao hivyo?

Hivyo tunapoliangalia suala la kufeli kwa wanafunzi tunapaswa kuliangalia kwa undani zaidi, kwani hata sasa tunaona zile shule zilizokuwa kongwe kwa kutoa matokeo mazuri nazo bado hazijafanya vizuri pia.

Hata shule za seminari na nyingine zisizokuwa za serikali nazo hazijafanya vizuri ukilinganisha na miaka ya nyuma. Wakati mwingine nafikiri kwamba hata suala la kudhibiti mitihani kuvuja nayo inaweza kuwa sababu kubwa ya kupata matokeo haya tuliyoyapata sasa.

Waziri Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo wamejitahidi katika kudhibiti kuvuja kwa mitihani, hivyo kwa hili ni lazima tuwapongeze.

Kwa kuwa ubora wa elimu inayotolewa katika nchi ni moyo wa taifa husika, ni vyema tukafanya utafiti wa kutosha kujua nini kinasababisha kuporomoka kwa elimu yetu na kamwe tusikimbilie majawabu rahisi kama kujiuzulu kwa Waziri na mengineyo ya kisiasa.

Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa gazeti hili

No comments:

Post a Comment