12 February 2013
Mkutano Mkuu wa Polisi uwe na jawabu la kukomesha uhalifu
JESHI la Polisi nchini, limekuwa na changamoto kubwa ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali
nchini ili kulinda usalama wa raia na mali zao.
Wakati jeshi hilo likitumia mbinu mbalimbali za kukabiliana na vitendo hivyo, wahalifu nao wamekuwa wakibuni mbinu mpya
siku hadi siku ili kufanikisha uhalifu waliopanga kuufanya.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, imesema leo Rais Jakaya Kikwete atafungua Mkutano Mkuu wa mwaka jeshi hilo ambao utashirikisha Maofisa Wakuu wa jeshi, makamanda wa mikoa
pamoja na vikosi.
Mkutano huo unafanyika mjini Dodoma na unatarajiwa kumalizika Februari 15 mwaka huu ambapo washiriki watapata fursa ya kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji.
Mambo hayo ni pamoja na utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa mwaka 2012 na kuweka mikakati ya namna ya kuendelea kudhibiti, kukabiliana na vitendo vya uhalifu nchini.
Katika mkutano huo, mada mbalimbali zitatolewa na wadau kutoka ndani na nje ya jeshi hilo ambazo zitalenga kuimarisha uwezo wa namna ya kuzuia, kupambana na kutanzua uhalifu nchini kuanzia
ngazi ya familia.
Sisi tunasema kuwa, mkutano huu ni muhimu sana kwa jeshi hilo katika kipindi hiki chenye changamoto kubwa inayotokana na aina ya uhalifu unaofanywa na wahalifu katika maeneo mengi nchini.
Upo umuhimu mkuwa wa washiriki kuelezea vikwazo ambavyo wanakumbana navyo katika kupambana na uhalifu wa kisasa ili wakufunzi waumize vichwa na kutoa majibu ya maswali yenu.
Ukweli ni kwamba, mbinu zinazotumiwa na wahalifu kufanikisha uhalifu waliodhamiria kuufanya ni kubwa sana hivyo tunaamini mkutano huu, utatoa majibu ya nini cha kufanya ili wahusika wa vitendo hivyo waweze kukamatwa bila kusababisha madhara
kwa wannchi wasio na hatia.
Leo hii idadi kubwa ya Watanzania wamepoteza maisha katika matukio mbalimbali ya uhalifu hasa yanayohusu mapambano ya kurushiana risasi kati ya wahalifu na polisi kwenye makazi ya watu.
Tumeshuhudia polisi wenye silaha nzito wakitumia nguvu kubwa kuwazuia waandamanaji wenye fimbo na kusababisha mauaji wakati nchi za wenzetu, zimepiga hatua kwa kuboresha mfumo wa utendaji kazi yanapotokea maandamano ya kisiasa au yale yanayohusisha wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu.
Upo umuhimu wa washiriki kukumbushwa wajibu wa kuzingatia kiapo chao kwa kuhakikisha kuwa, kazi wanazofanya siziwe mtaji wa kujinufaisha kwa kupindisha sheria.
Vitendo vya rushwa vinavyolalamikiwa kwa baadhi ya polisi, vinalichafua jeshi hilo mbele ya jamii, kuhatarisha amani na utulivu kama inavyosisitizwa na viongozi wetu siku hadi siku.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment