12 February 2013
Mkapa aomba kushushwa gharama za matibabu
Na Pendo Mtibuche, Dodoma
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, ambaye pia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Bw. Benjamini Mkapa, amesema ipo haja kwa Serikali, Mifuko ya Hifadhi za Jamii na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama kwenye kituo cha kusafisha damu chuoni hapo.
Alisema Watanzania wachache ndio wanaoweza kupata huduma
ya kusafishwa damu katika kituo mbalimbali kutokana na gharama zake kuwa kubwa hivyo wengi wao kushindwa kuimudu.
Bw. Mkapa aliyasema hayo chuoni hapo juzi wakati akizindua
kituo hicho na kusisitiza kuwa, uzinduzi huo ni mwanzo wa maandalizi ya upanuzi wa huduma usafishaji damu pamoja
na magonjwa ya figo.
“Kuwepo kwa kituo hiki hap chuoni ni faraja kubwa kwa wakazi
wote wa Kanda ya Kati na Tanzania kwa ujumla kwani kitasaidia
wagonjwa wengi na kuokoa maisha yao,” alisema Bw. Mkapa.
Aliongeza kuwa, ujenzi wa kituo cha uchunguzi wa magonjwa chuoni hapo na Chuo cha Afya ni sehemu ya maandalizi hivyo juhudi zinafanywa ili kutafuta wafadhili wa kutoa vifaa pamoja
na mashine zinazohitajika ili kufanikisha uanzishwaji na utoaji
wa huduma za tiba ya figo.
“Lengo la kutaka kuanzisha kituo hiki ni kutaka kiwe kitovu cha tiba ya figo katika hatua zote barani Afrika,” alisema.
Akizungumzia uanzishwaji wa kituo hicho, Bw. Mkapa alisema umetokana na msaada wa mashine 10 za Dialysis zilizotolewa na Dkt. Tokuda Torao wa Tukushukai Medical Corporation ya Japani kupitia Tanzania Tokuda Foundation.
Kituo hicho tayari kimeanza kufanya kazi na hivi sasa kina wagonjwa wanne na uwezo wake utakuwa kutoa huduma kwa wagonjwa 20 kwa siku hivyo mwaka mzima, kitaweza
kuhudumia zaidi ya wagonjwa 7,000.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi, alisema takwimu za wagonjwa wa figo nchini zinaongezeka kila mwaka kutokana na magonjwa hayo
kuchochewa na kisuakari pamoja na shinikizo la damu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment