12 February 2013
Ofisa Madini atuhumiwa kujipatia bil. 2.7/-
Na Patrick Mabula, Shinyanga
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameazimia kumkataa Ofisa Madini Mkazi wa Wilaya hiyo Bw. Tuna Bandoma, kwa tuhuma za kutumia madaraka yake kujinufaisha kupitia wachimbaji wadogo wa dhahabu na kujipatia
sh. bilioni 2.7.
Azimio hilo lilifikiwa mwishoni mwa wiki katika kikao cha
Baraza la Madiwani ambao walidai kuwa, Bw. Bandoma amekuwa akiwatumia wachimbaji hao kumchimbia dhahabu kwa zamu na kudai mapato yanayopatikana, hugawana viongozi wa Serikali ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini.
Katika hoja yake ya msingi, Diwani ya Kata ya Nyankende, Bw. Doa Magingi, alimtuhumu Bw. Bandoma kwa kuikosesha mapato halmashauri katika migodi ya wachimbaji wadogo aliowazuia wasitoe ushuru na kujinufaisha kwa masilahi binafsi.
Alisema Bw. Bandoma amejikusanyia fedha hiyo katika migodi
ya wachimbaji wadogo wa machimbo ya Nyangarata, Mwabomba, Busulwangili na mengine yaliyopo wilayani humo.
Akisoma taarifa ya Kamati ya Fedha , Uongozi na Mipango ya halmashauri hiyo mbele ya baraza, Diwani wa Kata ya Lunguya
Bw. Benedicto Manwali, alisema wamebaini Bw. Bandoma amejinufaisha kwa kujipatia sh. bilioni 2.7 katika miezi
mitano kuanzia Septemba 2012.
“Fedha hizi alijipatia kqatika mazingira haya...kwanza alizuia halmashauri isikusanye ushuru na baadaye aliwapa masharti wachimbaji katika migodi hiyo kufanya kazi ya zamu katika
masaa 12 za kumchimbia madini katika migodi yote na kila
baada ya siku tatu, dhahabu na mapato yote ni mali yake,”
alisema Bw. Manwali.
Diwani wa Kata ya Segese, Bw. Joseph Manyala, alisema kamati iliwauliza wachimbaji wadogo wakati wakimchimbia ofisa huyo na kudai Bw. Bandoma aliwaambia mapato yanayotokana na dhahabu hiyo anayagawa kwa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa, Wizara ya Nishati na Madini ili wasifukuzwe maeneo hayo.
Kutokana na tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Alfured Mhanganya, alimsimamisha Bw. Bandoma mbele ili kujibu hoja hiyo na kujitetea kuwa, yeye alikuwa anaombwa na viongozi wa Serikali na alikuwa akitumia utu wake.
Bw. Bandoma alidai kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo katika machimbo yote wilayani humo ili waweze kujipatia kipato hivyo anashangaa kuona madiwani wanamhukumu na kumkataa
kutokana na ubinadamua wake.
Pamoja na madiwani hao kuazimia kumkataa Bw. Bandoma, pia waliazimia kuundwa kwa tume kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya
hiyo ambayo itajumuisha baadhi ya madiwani na viongozi wa Serikali kuchunguza kwa kina tuhuma hiyo.
Walidai tuhuma hizo zinadaiwa kuwahusisha viongozi wa Serikali katika mgawo wa fedha zinazodaiwa kutoka kwa wachimbaji hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment