26 February 2013

Elimu ya teknolojia ya umeme jua ipelekwe vijijini



Na Godwin Msalichuma

UTOAJI elimu juu ya namna ya upatikanaji wa vifaa vya umeme jua na matumizi yake ni mkakati mzuri ambao wananchi wa vijijini wanaomba halmashauri zao kama zina watalaam waliobobea katika fani hiyo waende kuwapatia ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.

Wananchi katika vijiji vya halmashauri za Wilaya katika Mkoa wa Mtwara ambako mwandishi wa makala haya alitembelea mfano vijiji vya Mgao na Mbaye katika halmashauri ya Wilaya ya Mtwara vijijini akifanya habari za kiuchunguzi kuhusu nishati mbadala jinsi inavyoenea walimweleza kuwa kuna haja ya watalaam kufika huko ili wajue gharama na matumizi
sahihi ya aina hiyo ya umeme.

Watalaam wa umeme jua hapa nchini na wauzaji wa vifaa wako kwa hivi sasa na wanatoa elimu kwa wananchi watakaopenda kuipata lakini hawajafanikiwa kufika Maeneo ya vijijini huko waliko wananchi wengi ambao wanamahitaji ya nishati mbadala ili kupunguza madhara ya ukataji misitu na kuongeza muda wa kuzalisha mali mashambani.

Elimu hiyo itakuwa na manufaa kwa wananchi hao kwani watajua gharama za kupata nishati hiyo lakini pia wanaweza kuishauri Serikali kupitia halmashauri zao ziweze kupunguza ushuru katika vifaa hivyo ili waweze kupata na kutumia mbadala huo kwa gharama nafuu.

Bw.Edward Mkazi ni mwanakijiji wa mgao katika halmashauri ya Wilaya ya Mtwara vijijini anasema wakati nchi ikikabiliwa na tatizo sugu la upatikanaji wa nishati ya umeme Watanzania wametakiwa kubadilika na kuanza kujitokeza kwa wingi katika matumizi ya umeme wa mionzi ya jua na hili haliwezi likakamilika kama halmashauri hizitachukua hatua ya kuleta watalaam vijijini.

Anasema kuwa kwa anavyojua yeye kwa kudadisi kwake kuwa umeme huo wa mionzi ya jua ni umeme bora na hauna tofauti na umeme wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na jitihada zikifanyika na serikali kupitia halmashauri kuisambaza elimu ya matumizi ya nishati hii na kupunguza ushuru kwa wafanyabiashara wanaoingiza vifaa hivi na teknolojia kwa
ujumla matatizo ya umeme mjini na hata vijijini yatakwisha na kunusuru misitu yetu.

“Mimi sidhani kama Serikali inashindwa hili au kama watunga sera hapa nchini wanashindwa kuishauri vizuri juu ya nishati hii mbadala…… kwani nasikia umeme huu unaweza hata kuwasha pasi na jiko la kupikia” anasema Bw. Mkazi kwa mshangao mkubwa.

Bw.Kazimoto Shomari wa kijiji cha Mgao katika halmashauri hiyo anasema kwa habari anazozipata ambazo siyo rasmi kutoka kwa watalaam kuwa kwa kujiunga na umeme huo wanaweza kupunguza kero wanazozipata katika shuguli zao za kila siku nyumbani na kuweza kuokoa muda mwingi wa kufanya kazi shambani.

“Kwa habari ninazozipata mimi zisizo rasmi kutoka kwa watalaam wa nishati hiyo kuwa ukiweza kupata maunganisho ya umeme huo unapunguza kero za majumbani tunazozipata kutoka katika matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuongeza muda wa kufanya kazi shambani”anasema Bw. Shomari.

Mwandishi wa makala haha pia aliongea na kampuni ya makandarasi maalumu wa nishati hiyo ya jua, Mbecha General Supplies ya Mtwara mjini, ndio wasambazaji wa huduma hiyo ikiwa ni pamoja na uuzaji, na wanaweza kukupatia wafungaji wa vifaa na mitambo ya umeme huo wa jua katika halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Kwa kutaka kujua zaidi niliongea na mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Said Ramadhan, anaelezea teknolojia hiyo kwa undani zaidi hadi kumfikia mtumiaji ambapo anasema kwa upande wa matumizi ya kupikia bado ni changamoto kubwa siyo kuwa vifaa havipo bali gharama yake ni kubwa kiasi kwamba kwa mtu wa kijijini awe amejipanga vizuri.

Anasema teknolojia ya umeme wa jua ilianza kufanyiwa utafiti tangu miaka 1800 na utafiti huo ulianza kuzaa matunda katika miaka ya 1950,ambapo anasema matunda ya utafiti huu yalipata nguvu miaka ya 1970 katika nchi za Ulaya na Marekani kutokana na mgogoro wa mafuta.

Anabainisha zaidi kuwa hadi sasa umeme wa jua unatumika sehemu nyingi sana duniani na Ujerumani ndiyo inayoongoza katika matumizi ya nishati hiyo,anasema nishati ya umeme wa jua ni teknolojia ya uvunaji wa mwanga wa jua kupitia vifaa maalumu ambavyo hugeuza mwanga huo kuwa umeme.

Muunganiko wa vifaa hivi maalumu na vingine ndivyo vinavyounda mfumo kamili wa umeme huo wa jua. Mtaalamu huyo anatutajia aina ya vifaa vinavyounda mfumo kamili wa umeme wa jua.

Anavitaji vifaa hivyo ni Moduli ya sola (Solar Panel/Module) Bw.Ramadhani anasema hiki ni kifaa mama katika mfumo wa umeme huo ambapo muduli hupokea mionzi ya jua na kuibadilisha kuwa umeme.

Anatoa ufafanuzi kuwa aina moja huitwa kristalini ambayo huonekana kama kioo cha bluu , bluu-nyeusi chenye mistari iliyokatiza (draft),na aina nyingine huitwa amofasi huonekana kama kioo cheusi chenye mistari ilinyooka kuanzia juu kwenda chini.

Anabainisha kuwa vifaa vingine ni Betri ya sola (Solar Battery) anasema kuwa betri ya sola ni muhimu kwenye mfumo wa umeme huu kwani hii hutunza umeme unaonaozalishwa na module/panel ya sola wakati jua linawaka kwa ajili ya matumizi ya wakati ambao mwanga wa jua haupo (usiku/mawingu mazito).

Vile vile anaongeza kuwa kuna Kidhibiti chaji (Solar Regulator),anasema hii ndiyo akili ya mfumo wa umeme huu wa jua ambapo huhakikisha betri inapokea umeme unaolingana na uwezo wake tu na si zaidi, pia huhakikisha betri haitumiki zaidi ya chini ya kiwango kilichokadiriwa kitaalamu, hivyo kuifanya betri hiyo idumu kwa muda mrefu, pia humsaidia mtumiaji kuelewa mwenendo wa mfumo wake wa umeme
huo wa jua.

Kuna kigeuza mkondo (Inverter) Mtendaji huyo anazidi kufafanua kuwa umeme unaozalishwa na sola ni sawa na ule wa betri yaani volti 12,hivyo huwezi kutumia moja kwa moja vifaa vinavotumia umeme wa TANESCO,yaani wa volti 240, hivyo basi Inveta hubadilisha umeme wa betri wa volti 12 kuwa sawa na ule wa TANESCO wa volti 240 ili uweze kutumia vifaa vyako vinavyohitajika kama wa TANESCO ili viweze kuwaka.

Aidha aliendelea kutaja kifaa kingine ambacho ni kishika moduli ya sola (Solar Mounting Structure) anasema hii ni fremu ya kufungia moduli ya sola, hutengenezwa katika vipimo maalumu ili moduli ya sola ikifungwa iweze kumulikwa na mwanga wa jua kuanzia asubuhi hadi jioni na katika majira yote ya mwaka, anasema kuwa pamoja na vifaa hivyo
vilivyoorodheshwa, mfumo wa sola hukamilishwa na vifaa vingine vya ziada kama waya, swichi na soketi.

Katika matumizi ya umeme wa jua mwandishi aliongea na mtalaam mwingine katika kampuni hiyo Bw. Hassan Said na anasema umeme huu hutumika kuwasha vifaa mbalimbali vinavyotumia umeme wa betri au ule wa TANESCO ambapo umeme huu pia hutumika kuwasha taa, redio, runinga, vifaa vya
mawasiliano, chaji ya simu na vinginevyo.

Pia umeme huu hutumika mahala popote pale kama vile majumbani,zahanati, vituo vya afya, shuleni ofisini na mashambani ambapo unaweza kuleta mapinduzi ya kimaendeleo haswa sehemu za vijijini ambako bado gridi ya taifa haijafika huko.

Anasema kuwa umeme huu ni rafiki wa mazingira, kwani hautoi moshi,hauna kelele, hautumii mafuta yoyote na wala hauna matengenezo ya mara kwa mara kama ilivyo kwa jenereta, pia hakuna malipo ya kila mwezi kama ule wa TANESCO.

Aidha, wao wanakufanyia ukadiriaji wa kiwango cha umeme
kinachohitajika kwa matumizi ya vifaa vyako na kukupa makadirio ya gharama zake mara unapotoa maelezo ya mahitaji yako, Bw. Said anasema watakushauri ufungiwe mfumo wako kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu na miiko yake huku wakikuwekea kipaumbele cha usalama kwa watumiaji na vifaa vyao.

Kwa wateja wanaotoka nje ya Manispaa ya Mtwara, hawana haja ya kusumbuka hadi katikati ya mji kwenye msongamano mkubwa wa watu kutafuta huduma ya nishati hiyo.

Aidha anatoa wito kwa wananchi wote kuwa vifaa vya umeme jua vipo na vimeondolewa ushuru na kodi kwa hivyo gharama yake siyo kubwa ukilinganisha na umeme mwingine unaozalishwa kwa kutumia aina nyingine ya vyanzo tofauti na jua.

No comments:

Post a Comment