12 February 2013
Meatu wapinga kilimo cha mkataba
Na Suleiman Abeid,Meatu
BAADHI ya madiwani na wakazi wakazi wa wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wameendelea kupinga suala la kilimo cha mkataba kwa madai kuwa hakina tija kwa wakulima na badala yake kimelenga kuwageuza kuwa watumwa wa wafanyabiashara wa zao la pamba.
Hatua ya wakazi hao inatokana na hoja iliyotolewa hivi karibuni katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) ambapo walisema pamoja na Serikali kuhimiza suala la kilimo cha mkataba lakini haijafanya utafiti wa kina kuona jinsi kilimo hicho kitakavyomnufaisha mkulima.
Akichangia hoja katika kikao hicho,Diwani wa kata ya Mwabuzo (CCM),Seni Challya alisema katika kipindi kifupi tangu zilipoanza kampeni za kuwataka wakulima hasa wale wa zao la pamba kujiunga na utaratibu wa kilimo cha mkataba wakulima wengi wamebaini utaratibu huo haufai.
Challya alisema kilimo cha mkataba kimeonekana wazi kutokuwa na maslahi yoyote kwa mkulima na badala yake kitasababisha wakulima wengi kugeuka kuwa watumwa wa kuwatumikia wafanyabiashara wa zao la pamba watakaokuwa wamefunga mikataba ya wakulima wa zao hilo.
“Mwenyekiti suala la kilimo cha mkataba bado haliungwi mkono na wakulima wengi, lina changamoto nyingi, wapo wale ambao wamejaribu mwaka jana, wameona wazi hakifai, maana wengi walitegemea watanufaika hasa upande wa bei, lakini ajabu msimu ulipofika bei ya pamba ilikuwa sawa kwa wote, wenye mkataba na wasio na mkataba,”
“Lakini hata upande wa wafanyabiashara wenyewe wapo ambao wameanza kulalamika baada ya wakulima kushindwa kuwalipa fedha za pembejeo walizokuwa wamekopeshwa, hii inasababishwa na mavuno kuwa haba kinyume na walivyotarajia, sasa wakulima hawa wanalazimika kulipa deni hilo katika msimu ujao, je huu si utumwa?” alihoji Challya.
Kwa upande wake Kimwaga Jackson alisema iwapo Serikali italazimisha suala la kilimo cha mkataba ni wazi itawasababishia wakulima wengi wageuke kuwa maskini katika nchi yao kutokana na mikataba kutoeleza wazi pale linapotokea suala la ukame hasara italipwaje.
Jackson alisema kwa mujibu wa mikataba ya hivi sasa iwapo mkulima atashindwa kufikia kiwango cha kilo za pamba alizotakiwa kuzalisha ili kumfidia mfanyabiashara aliyemkopesha pembejeo za kilimo atatakiwa kulipa deni hilo katika msimu utakaofuata bila kutegemea tena kupewa pembejeo nyingine na mtu aliyefunga naye mkataba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment