20 February 2013

Balozi Kamala aula Ubeligiji



Na Mwandishi Maalum, Ubeligiji

BALOZI wa Tanzania nchini Ubeligiji, Dkt. Diodorus Kamala, ameteuliwa na mabalozi wenzake wa Afrika wanaoziwakilisha
nchi zao nchini humo, kuwa Mwenyekiti wao.


Awali nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Balozi wa Swaziland, Bw. Joel Nheleko ambaye amemaliza muda wake ambapo Balozi Kamala atashikilia wadhifa huo miezi sita hadi Julai mosi mwaka huu.

“Nimefurahi kupewa heshima hii, nitaitumia vizuri nafasi hii
kuvutia fursa za uwekezaji nchini Tanzania,” alisema.

Wakati huo huo, juzi mabalozi wa nchi tano zinazozunguka
Bonde la Ziwa Tanganyika, walimchagua Balozi Kamala
kuwa Mwenyekiti wao.

Nchi wanachama zinazozunguka bonde hilo ni Burundi, Rwanda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Zambia ambapo nchi hizo zimeunganisha nguvu kutafuta wafadhili kwa
ajili ya maendeleo ya bonde hilo.

Mabalozi hao wamedhamiria kuliendeleza bonde hilo lenye
wakazi wasiopungua milioni 40 kwa kujenga miundombinu,
kurahisisha usafiri na usafirishaji, kujenga reli mpya na
kuendeleza utalii.
Chini ya mpango huo, mabalozi hao wamepanga kuboresha viwanja vya ndege vya nchi wanachama vya Mbala, Kalemie, Bujumbura, Kigoma na Kasanga ili kurahisisha usafiri wa anga katika ukanda huuo.

Dk. Kamala amekabidhiwa jukumu la kuratibu mpango huo ambapo mabalozi hao watatafuta fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya mradi huo.

No comments:

Post a Comment