21 January 2013

Wanachama Yanga wampa rungu Manji *Nsajigwa alamba mil. 1 nidhamu bora




Na Zahoro Mlanzi

WANACHAMA zaidi ya 1444 wa Klabu ya Yanga, wameridhia kumpa ridhaa Mwenyekiti wao, Yusuph Manji pamoja na Makamu wake, Clement Sanga kuteua Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaowataka wao pamoja na kumfukuza mjumbe yeyote atakayeonekana hafai.


Uamuzi huo ulifikiwa jana wakati wa Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa klabu hiyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja baada ya Manji kuomba kurekebisha katiba ya klabu hiyo ambapo sasa mwenyekiti huyo atakuwa na haki ya kuchagua wajumbe wake  wa kamati ya utendaji na si kwa kupigiwa kura kama iliyokuwa awali.

“Naomba mpango huu uanze kuanzia sasa kwa kuwa kumekuwa na shida ya wajumbe kutokubaliana na sisi mara baada ya kuchaguliwa,”alisema na kuongeza;

"Mfano ni mjumbe wa kamati hiyo kuwageuka wenzake mara baada ya timu hiyo kuweka kambi nchini Uturuki na kudai kuwa hawewezi kufanikiwa kama timu itakuwa ikigawanyika.

Alisema kuna wajumbe wengine wapo katika uongozi lakini hana imani nao kwani wamekuwa wakiwageuka na ndio maana akaomba ridhaa amchukulie hatua mjumbo huyo.

Katika hatua nyingine, beki wa timu hiyo, Shadrack Nsajingwa amezawadiwa sh. milioni moja kwa kuonyesha nidhamu na kudumu muda mrefu katika klabu hiyo.

Nsajigwa alikabidhiwa zawadi hiyo wakati wa mkutano huo na Manji pamoja na Mwenyekiti wa  Kamati ya Mashindano, Abdallha Bin Kleb akipewa zawadi ya kuisaidia timu hiyo.

Akikabidhi zawadi hiyo, Manji alisema wameamua  kutoa zawadi kwa Bin Kleb kutokana na mchango wake mkubwa anaoufanya kwa timu na pia Nsajigwa kwa kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu huku akionesha nidhamu nzuri.

Wakati huohuo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alisema timu hiyo inatarajiwa kushuka uwanjani, Jumatano kurudiana na Black Leopard, mchezo huo umepangwa kufanyika jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM, Kirumba.

No comments:

Post a Comment