04 January 2013
Wafugaji wamvamia Kiongozi wa Kanisa, kumpiga mapanga
Na Rashid Mkwinda, Mbeya
SIKU moja baada ya Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athumani, kudai jeshi hilo limefanikiwa kutatua mgogoro wa wakulima na wafugaji, Katekista wa Kanisa Katoliki Kigango cha Uturo, Parokia ya Chosi, wilayani Mbarali, Angelo Mvimba (49) amevamiwa, kukatwa na mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa wafugaji.
Katekista huyo alivamiwa na kundi la watu wasiopungua sita ambao alikutana nao wakiwa na kundi la ng’ombe wakitaka kulisha mifugo yao katika shamba la Kanisa lililopo Kijiji cha Uturo.
Akizungumzia na gazeti hili, Katekista Mvimba ambaye amevunjika mkono wa kulia, kujeruhiwa kichwani, mbavuni na kitu chenye ncha kali, alisema siku ya tukio alikuwa akitoka kuangalia mbegu za mpunga kwenye kitalu cha shamba la Kanisa majira ya mchana.
“Nilivamiwa na mafugaji ambao walikuwa na kundi la ng'ombe ambao walinipiga na kunijeruhi, kichwani, mbavuni na kunivunja mkono wa kiume hadi nikapoteza fahamu,” alisema.
Alisema wasamalia waliopita eneo hilo, walimkuta akiwa amepoteza fahamu hivyo walimchukua na kumkimbiza Hospitali ya Misheni Chimala ambako alipatiwa matibabu, kushonwa nyuzi 14 kichwani na kuruhusiwa Desemba 31,2012.
“Nilijikuta nimelazwa katika Hospitali ya Misheni Chimala nikiwa na majeraha kichwani na mbavu zinauma sana, wasamaria wema waliniokota eneo la tukio na kunipeleka hospitali,” alisema.
Alisema watu wengine waliovamiwa na watu hao ni Bw. Titus Sanga ambaye alipigwa na kuporwa simu yake ya mkononi, Bw. Patrick Mahenge na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la
Mwangono.
“Hivi sasa wakulima wa Vijiji vya Uturo, Mtamba na Ukwama wanaishi kwa hofu kutokana na uvamizi wa kundi la wafugaji ambao wanazuia wananchi kulima na kumwagilia mashamba
yao nyakati za jioni,” alisema Katekista Mvimba.
Aliongeza kuwa, kipindi hiki wakulima wa maeneo hayo wanaogopa kwenda mashambani wakihofia usalama wa maisha yao baada ya wafugaji kuyateka mashamba na kuyafanya malisho ya mifugo.
Juzi Kamanda Athuman alisema, kuwa tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji limepatiwa ufumbuzi ambapo mwaka
2012, hakuna tukio kubwa lililoripotiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment