31 January 2013

Wabunifu 25 kushiriki Lady in Red



Na Mwali Ibrahim

WABUNIFU 25 nchini, wanatarajia kuonesha mavazi katika mashindano ya Lady in Red 2013, yanayotarajia kufanyika Februari 9 mwaka huu katika Ukumbi wa Serena Hoteli, Dar es Salaam.


Onesho hilo ni maalumu kwa ajili ya kuwainua wabunifu wachanga, ambao watapata nafasi ya kuonesha mavazi yao, ikiwa ni pamoja na kuchangisha fedha za kumalizia ujenzi wa kituo cha Kikale cha kutunza watu walioathirika na dawa za kulevya kilichopo Rufiji mkoani Pwani.

Mkurugenzi wa Fabak Fashions ambao ndiyo waandaaji wa maonesho hayo, Asia Idarous aliwataja wabunifu hao Dar es Salaam jana kuwa ni Mustafa Hassanali, Khadija Mwanamboka, Ally Remtula, Salim Ally, Catherine Mlowe na Yvone Peter.

Wengine ni Jackson Gumbala, Naila Yusuph, John Kapalata, Faustin Simon, Maangaza Nyange, Lucky Creation, Nadwan, Augusta, Masaki, Hamid Abdul, Annete Ngongi, Bahaia, Natasha, Ailinda Sawe, Naima Msika, Jabeer, Benedict Christopher na Halima Kamusi.

"Tumeamua kulenga kuwasaidia wabunifu wachanga kutokana na kuwepo wabunifu wengi, ambao wana vipaji na hawatambuliki hivyo itakuwa ni fursa yao kuonesha vipaji vyao, kwa watu watakaohudhuria siku hiyo," alisema.

Alisema siku hiyo, pia kutakuwa na mnada ambapo gauni la Miss Tanzania 2012 Brigitte Alfred, alilolivaa mwaka jana wakati akitwaa taji hilo litauzwa.

Mkurugenzi huyo alisema pia katika maonesho hayo, kutauzwa bidhaa zitakazotolewa na Kampuni ya nywele ya Darling, ili kupata fedha za kuendeleza ujenzi wa kituo hicho.

Alisema ujenzi wa kituo hicho cha Kikale, upo katika hatua za mwisho na kitaanza kutoa huduma mwishoni mwa Februari au mwanzoni mwa Machi mwaka huu, ambapo tayari kuna vijana wanaoutumia dawa za kulevya, wameomba kujiunga, ili kupatiwa ushauri.

Katika kunogesha usiku wa Lady in Red siku hiyo, kutakuwa na burudani itakayoporomoshwa na bendi ya muziki wa dansi ya Kalunde.

Asia alisema kiingilio kitakuwa sh. 20,000 na sh. 50,000, ambapo tiketi zinapatikana katika ofisi za Fabak Fashions Mikocheni na Serena Hotel.

No comments:

Post a Comment