21 January 2013
Viongozi mitaa,watendaji wailalamikia serikali
Na Darlin Said
VIONGOZI wa Serikali za mitaa na Watendaji wameilalamikia serikali kushindwa kuwashirikisha katika kufanya maamuzi mbalimbali ya kimaendeleo hali inayosababisha kutokuwa na uhusiano nzuri baina yao na wananchi.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na baadhi ya wenyeviti,wajumbe wa serikali za mitaa katika mkutano ulioandaliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Agenda Participation 2000.
Katika mkutano huo Mwenyekiti wa Serikali za mitaa kutoka mtaa wa sunna uliopo Tandika Bw.Ridwani Hemed alisema tabia ya manispaa kupanga mambo ya maendeleo bila kuwashirikisha inasabisha chuki kwa wananchi, kwani inapotokea kutoridhishwa na maamuzi yaliyofanywa na viongozi kutoka ngazi za juu lawama zinakuja kwa viongozi wa ngazi za chini .
Hivyo alitoa wito kwa Ofisi za manispaa kuwashirikisha viongozi hao ili inapotokea tatizo kwa wananchi juu ya serikali yao wawe na uwezo wa kujitetea.
Naye Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa kutoka Kinondoni, Bi.Amina Mtemvu alisema viongozi wa ngazi za chini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na ofisi maalum pamoja na vyanzo halisi vya mapato.
Alisema kutokana na hali hiyo inalazimika kuwachangisha wananchi ili waweze kupata fedha za kuendesha ofisi ikiwemo vifaa vya ofisi vitendea kazi vya usafi.
Alisema katika ukusanyaji ushuru ofisi hizo huwa hazishirikishi na badala yake kazi hiyo inafanywa na manispaa baada ya hapo fedha hizo hizo hazitumiki kwa ajili ya maendeleo ya mtaa wao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa asasi hiyo Bw.Moses Kulaba alisema lengo la mkutano huo ni kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi za chini wa serikali za mitaa katika kufanya kazi zao.
Alisema katika mikutano iliyopita wamebaini kutokuwa na uhusiano nzuri baina ya watendaji wa serikali za mitaa na viongozi wa siasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment